Maelfu waandamana Indonesia kulaani jinai za Israel dhidi ya Wapalestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i70314-maelfu_waandamana_indonesia_kulaani_jinai_za_israel_dhidi_ya_wapalestina
Maelfu ya wananchi wa Indonesia wameandamana ambapo mbali na kutangaza kuwaunga mkono wananchi wa Palestina wamelaani pia jinai za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya wananchi hao wasio na hatia.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
May 19, 2021 06:54 UTC
  • Maelfu waandamana Indonesia kulaani jinai za Israel dhidi ya Wapalestina

Maelfu ya wananchi wa Indonesia wameandamana ambapo mbali na kutangaza kuwaunga mkono wananchi wa Palestina wamelaani pia jinai za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya wananchi hao wasio na hatia.

Maandamano hayo makubwa yalifanyika jana ambapo waandamanaji wakiwa wamebeba mabango na maberamu walikusanyika mbele ya ubalozi wa Marekani mjini Jakarta na kuonyesha upinzani wao kwa hujuma na mashambulio ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina na Ukanda wa Gaza.

Waandamanaji hao wamemtaka Rais wa Marekani Joe Biden ambaye nchi yake imekuwa ikiuunga mkono utawala dhalimu wa Israel asitishe mara moja unyama huo wa Israel ambao hadi sasa umeuwa shahidi zaidi ya Wapalestina 200.

Maandamano hayo yalihudhuriwa na wananchi wa matabaka mbalimbali wakiwemo wanachuo, vijana, wanachama wa jumuiya za kiraia, muungano wa wafanyakazi na kadhalika.

 

Tangu siku ya Jumatatu ya tarehe 10 Mei, jeshi la utawala ghasibu wa Kizayuni wa Israel limeanzisha mashambulio ya kinyama dhidi ya Wapalestina wa eneo la Ukanda wa Gaza, ambapo hadi sasa Wapalestina wasiopungua 220, wakiwemo watoto 63 wameshauawa shahidi kutokana na mashambulio hayo na wengine zaidi ya 1,500 wamejeruhiwa.

Katika kujibu uchokozi na jinai hizo za kinyama za utawala haramu wa Israel dhidi ya Gaza, makundi ya muqawama ya Palestina yamevurumisha mamia ya makombora kuelekea miji na vitongoji haramu vya utawala ghasibu wa Kizayuni katika ardhi za Palestina unayoikalia kwa mabavu.