Mrithi wa zamani wa kiti cha ufalme Saudia anateswa vibaya sana
-
Muhammad bin Nayef
Muhammad bin Nayef, mrithi wa zamani wa kiti cha ufalme aliyefutwa kazi ameteswa vibaya sana gerezani kiasi kwamba hana uwezo wa kutembea na ananyimwa dawa za kupunguza maumivu.
Muhammad bin Nayef alikuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia baina ya mwaka 2015 hadi Juni 2017 wakati alipouzuliwa kwa amri ya Mfalme Salman bin Abdulaziz na kisha nafasi yake kuchukulwa na mwanae mfalme huyo, Mohammad bin Salman.
Mnamo Machi 2020, Mohammad bin Nayef na mjomba wake, Ahmad bin Abdulaziz walikamatwa na kufungwa jela kwa tuhuma za uhaini.
Kanali ya televisheni ya NBC ya Marekani imechapisha ripoti kuwa, Muhammad bin Nayef ameteswa sana kizuzini kiasi kwamba anahitaji msaada kutembea.
NBC imenukulu duru za kuaminika zikisema kuwa Bin Nayef anashikiliwa katika jengo moja la ufalme karibu na Kasri ya Al Yamamah mjini Riyadh. Kasri hii ni makao makuu ya Mfalme wa Saudi Arabia.
Duru zinaarifu kuwa Muhammad bin Nayef amepungua kilo 23 na mikono yake imejeruhiwa vibaya kutokana na mateso aliyopata na wala hana ruhusa ya kuonana na daktari wake binafsi wala mawakili.
Muhammad bin Nayef alikamatwa Novemba 2017 huku akiwa amevuliwa nyadhifa zake zote alizokuwanazo hapo awali.
Hatua ya Mfalme Salman bin Abdulaziz ya kumuuzulu na kumfunga jela Mohammed bin Nayef na kumuweka mahala pake mwanawe Muhammad bin Salman imeshadidisha mivutano na vita vya kuwania madaraka nchini humo.