Algeria: Hakuna amani bila ya kuundwa nchi huru ya Palestina
-
Ramdane Lamamra
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Algeria amesema kuwa taifa la Palestina linataka amani na kwamba jambo hilo halitatimia bila ya kuundwa nchi huru ya Palestina.
Ramdane Lamamra amesema kuwa malengo matukufu ya ukombozi wa Palestina ni sawa na nguzo inayokusanya pamoja na kuimarisha ushirikiano baina ya mataifa ya Waarabu.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Algeria amezungumzia pia eneo la Miinuko ya Golan la Syria iliyovamiwa na kukialiwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel na kusema kuwa, jamii ya kimataifa inapaswa kuwajibika na kutekeleza majukumu yake kuhusu ukombozi wa eneo hilo la Syria linalokaliwa kwa mabavu na Israel.
Israel inaendelea kukalia kwa mabavu ardhi ya Palestina na Miinuko ya Golan ambayo ni sehemu ya ardhi ya Syria kutokana na himaya ya Marekani na misaada ya kisiasa na kiuchumi ya nchi za Magharibi.
Itakumbukwa pia kwamba, tarehe 10 Mei, utawala dhalimu wa Israel ulianzisha vita dhidi ya Wapalestina katika maeneo ya Ufukwe wa Magharibi na Ukanda wa Gaza, lakini kinyume na ulivyotarajia, ulikabiliwa na jibu kali la mashambulio ya makombora ya wanamuqawama wa Palestina; na baada ya jeshi la utawala huo kushindwa kukabiliana na muqawama, sambamba na miito ya mtawalia iliyotolewa na baraza lake la mawaziri kutaka vita visimamishwe, hatimaye mnamo tarehe 21 Mei utawala huo haramu ulihitimisha jinai zake za kinyama dhidi ya Wapalestina.