Umoja wa Mataifa waitaka Israel iache kubomoa nyumba za Wapalestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i72198-umoja_wa_mataifa_waitaka_israel_iache_kubomoa_nyumba_za_wapalestina
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameutaka utawala ghasibu wa Israel usitishe hatua zake za kubomoa nyumba na makazi ya wananchi wa Palestina
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Jul 10, 2021 03:09 UTC
  • Umoja wa Mataifa waitaka Israel iache kubomoa nyumba za Wapalestina

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameutaka utawala ghasibu wa Israel usitishe hatua zake za kubomoa nyumba na makazi ya wananchi wa Palestina

Stephane Dujarric, msemaji wa Antonio Guterres amesisitiza katika taarifa aliyoitoa mbele ya waandishi wa habari kwamba, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ana wasiwasi mkubwa na sera za bomoa bomoa na uharibifu wa mali za Wapalestina zinazofanywa na utawala vamizi wa Israel katika vijiji vya Hamsa al-Baqi'a na Aghwar huko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuelezwa kuwa, hatua hizo ni kinyume kabisa na sheria za kimataifa.

Siku tatu zilizopita na ikiwa ni mara ya saba mtawalia, wanajeshi wa utawala dhalimu wa Israel walivamia kitongoji cha Hamsa al-Baqi'a na kukibomoa ili kuwalazimisha Wapalestina wa eneo hilo wahame na hivyo kuandaa uwanja wa kupora ardhi hiyo na kujenga kitongoji cha walowezi wa Kizayuni.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

 

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, mwaka uliopita wa 2020 utawala wa Kizayuni wa Israel uliebomoa nyumba karibu 689 katika Ukingo wa Magharibi na Quds tukufu na kulazimisha mamia ya familia za Wapalestina kuwa wakimbizi.  

Utawala huo haramu umeendelea kubomoa nyumba na makazi ya Wapalestina licha ya Baraza ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutoa azimio nambari 2334 tarehe 23 Disemba mwaka 2016 ambalo liliutaka utawala huo kukomesha mara moja shughuli zote za ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi zote za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.