Nukta muhimu kuhusu kikao cha Baghdad
Kongamano la Baghdad Kwa Ajili ya Ushirikiano lilifanyika Jumamosi Agosti 28 na kushirikisa viongozi kutoka nchi 9 ambazo ni Ufaransa, Iran, Misri, Saudi Arabia, Uturuki, Qatar, Jordan, Kuwait na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Kuna nukta kadhaa muhimu kuhusu kongamano hilo.
Kwanza ni kuwa kikao hicho kilifanyika kwa lengo la kuwavutia wawekezaji na kutoa misaada ya kiuchumi kwa Iraq. Hata hivyo inaelekea kuwa malengo yaliyokusudiwa katika kikao cha Baghdad hayakuweza kufikiwa kwa sababu washiriki hawakutoa ahadi zozote. Weledi wengi wa masuala ya kisiasa ya Iraq walikuwa wameshatabiri kuwa kikao hicho hakingekuwa na mafanikio yoyote ya kiuchumi.
Nukta ya pili ni kuwa, inaelekea lengo muhimu zaidi la kikao hicho lilikuwa ni kutunisha misuli Waziri Mkuu Mustapha al Kadhimi na kuonyesha uwezo wake na wa waitifaki wake. Al Kadhimi amefanya jitihada kubwa kuongeza uungaji mkono wake nchini Iraq ili aweze kuchaguliwa tena kuwa waziri mkuu baada ya uchaguzi wa Oktoba. Kikao hicho kilifanyika zikiwa zimesalia siku 40 kabla ya uchaguzi na hivyo lengo lilikuwa ni kuonyesha kuwa Al Kadhimi ana uungaji mkono wa kigeni pia.
Nukta ya tatu ni kuwa kikao hicho kimeonyesha namna Iraq inavyotaka kuhuisha nafasi na hadhi yake katika eneo. Washiriki katika kikao hicho waliweza kuonyesha kuwa Iraq ni dola lenye nafasi muhimu katika masuala ya amani na upatanishi baina ya nchi za eneo zinazozozana.
Katika kikao hicho cha Jumamosi, Amir wa Qatar na Waziri Mkuu wa Imarati na pia Rais wa Misri na Amir wa Qatar walikutana na kufanya mazungumzo. Hizo ni nchi ambazo zimekuwa na hitilafu baina yao miaka ya karibuni. Kwa hivyo katika kikao cha Baghdad, Al Kadhimi alitaka kuonyesha kuwa Iraq ni dola muhimu ambalo linaweza kuwa kituo cha mazungumzo baina ya mahasimu wa eneo. Ni kwa msingi huo ndio washiriki wa kikao cha Baghdad wakaishukuru Iraq kwa ubunifu huo wa upatanishi.
Nukta ya nne ambayo tunaweza kuiashiria hapa ni kushiriki Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa katika kikao hicho cha Baghdad. Macron ni kiongozi pekee wa Magharibi aliyeshiriki katika kikao hicho. Hivyo inaonekana alishiriki katika mkutano huo ikiwa ni katika mkakati wa Ufaransa wa kujaribu kuhuisha nafasi ya ushawishi wake katika eneo. Mwezi Agosti mwaka jana Macron pia alitembelea Beirut mara mbili kwa lengo la kujaribu kutatua mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo.
Na nukta ya tano ni kuwa, washiriki wa kikao cha Baghdad walisisitiza kuhusu ulazima wa kuaminiana nchi za eneo, na kuwepo mazungumzo ili kupunguza hitilafu. Wakati huo huo, Fouad Hussein, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq amesema Syria haikualikwa katika kikao hicho kwa sababu baadhi ya washiriki hawakuafiki. Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu amezungumza katika kikao hicho cha Baghdad na kusema kuna haja ya kuhitimisha migogoro ya kieneo.
Kwa hivyo, inaelekea kuwa, kikao cha Baghdad kinaweza kuimarisha mshikamano wa eneo la Asia Magharibi na nukta hii ni muhimu sana.