Msemaji wa Taliban: Kushindwa Marekani Afghanistan ni funzo kwa wavamizi
Msemaji wa kundi la Taliban Zabuhullah Mujahid amesema kushindwa Marekani nchini Afghaniastan ni 'funzo' kwa wavamizi.
Katika mahojiano maalumu na Press TV mara baada ya askari wa mwisho kuondoka Afghanistan Mujahid amesema: "Kuondoka wavamizi Afghanistan ni siku ya furaha kwa watu wa Afghanistan na uhuru wao."
Ameongeza kuwa hii ni siku ambayo wavamizi wanapaswa kupata funzo kuwa hawakupaswa kutenda jinai wazlizotenda ambazo zimepelekea waondoke kwa fedheha.
Akizungumza mapema katika uwanja wa ndege wa Kabul, Mujahid amesema Taliban inataka kuwa na uhusiano mwema na nchi zote za dunia ikiwemo Marekani.
Kuwepo kijeshi Marekani na waitifaki wake huko Afghanistan kwa muda wa miaka ishirini hakujakuwa na matunda yoyote ghairi ya kuzidisha ugaidi, vita, hali ya mchafukoge na kuuliwa makumi ya maelfu ya wananchi wa Kiafghani.
Jumapili tarehe 15 mwezi huu serikali ya Rais Ashraf Ghani ilisambaratika na kiongozi huyo kuikimbia nchi baada ya Taliban kuingia Kabul mji mkuu wa Afghanistan. Wachambuzi wa mambo wanasema, hatua ya wanamgambo wa Taliban ya kuudhibiti mji wa Kabul imehitimisha uvamizi wa miaka 20 wa Marekani na nchi nyingine za Magharibi kwa kisingizio cha kuijenga upya Afghanistan. Aghalabu ya viongozi na wananchi wa Afghanistan wanaamini kuwa, hali ya sasa ya nchi hiyo ni matokeo ya siasa zilizofeli za Marekani nchini humo.