Umoja wa Mataifa: Afghanistan inakaribia kukumbwa na maafa ya kibinadamu
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuwa, Afghanistan inakaribia kutumbukia katika janga la kibinadamu.
Antonio Guterres, sambamba na kuashiria kushtadi mgogoro wa kibinadamu na kiuchumi na kusambaratika sekta ya utoaji huduma nchini Afghanistan amesema kuwa, hali inavyoonekana ni kuwa, nchi hiyo inaelekea kukumbwa na maafa ya kibinadamu.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, hivi sasa nusu ya wananchi wa Afghanistan wanahitajia misaada ya kibinadamu ili waweze kuendelea kuishi.
Sehemu nyingine ya taarifa hiyo ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa inaeleza kuwa, hivi sasa wanaume, wanawake na watoto wa Afghanistan wanategemea zaidi misaada ya jamii ya kimataifa kuliko wakati mwingine wowote ule.
Antonio Guterres pia amezitakka na kuzihimiza nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa "kutoa fedha za kutosha na zenye kukidhi mahitaji" kwa raia wa Afghanistan ambao hivi sasa wapo katika hali ngumu.
Jumapili tarehe 15 mwezi uliopita wa Agosti serikali ya Rais Muhammad Ashraf Ghani ilisambaratika na kiongozi huyo kuikimbia nchi baada ya Taliban kuingia Kabul mji mkuu wa Afghanistan. Wachambuzi wa mambo wanasema, hatua ya wanamgambo wa Taliban ya kuudhibiti mji wa Kabul imehitimisha uvamizi wa miaka 20 wa Marekani na nchi nyingine za Magharibi kwa kisingizio cha kuijenga upya Afghanistan. Aghalabu ya viongozi na wananchi wa Afghanistan wanaamini kuwa, hali ya sasa ya nchi hiyo ni matokeo ya siasa zilizofeli za Marekani nchini humo.