Rais wa Lebanon: Hizbullah ni mwakilishi wa Walebanon wote
Rais Michel Aoun wa Lebanon amesisitiza kuwa harakati ya Hizbullah inahesabiwa kuwa ni mwakilishi wa watu wa Lebanon na haijatenda kosa lolote.
Rais Aoun ametoa sisitizo hilo katika mahojiano maalumu na televisheni ya Aljazeera na akafafanua kuwa, hadi sasa hakuna tukio lolote la kutishia usalama lililosababishwa na Hizbullah ndani ya ardhi ya Lebanon na kwamba harakati hiyo ya muqawama inaheshimu sheria zote za nchi.
Rais wa Lebanon amebainisha kuwa, Hizbullah haijamdhuru raia yeyote wa kigeni hata wa nchi inayoitangaza harakati hiyo kuwa ni ya kigaidi na kwamba raia wote wa kigeni wanaotembelea Lebanon wanakuwa na usalama kamili.
Alipoulizwa katika mahojiano hayo, kama endapo Saudi Arabia itamtaka achukue hatua dhidi ya Hizbullah atafanyaje, Michel Aoun amejibu kuwa, Hizbullah inawakilisha theluthi moja ya watu wa Lebanon na haijatenda kosa lolote na ikiwa Riyadh itazungumzia suala hilo bila shaka yoyote litakataliwa na Lebanon.
Uhusiano wa Lebanon na Saudi Arabia umeharibika vibaya nadra kuwahi kushuhudiwa, baada ya waziri wa habari wa Lebanon George Kordahi kutoa matamshi ya kuliunga mkono taifa la Yemen na kulaani jinai zinazofanywa na Saudia dhidi ya watu wa nchi hiyo.
Sambamba na kukosoa uvamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen uliofanywa na muungano unaoongozwa na Saudi Arabia, Kordahi amesema, harakati ya Ansarullah haijavamia mahali popote na inachofanya ni kuwahami watu wake wanaoshambuliwa na ndege za kivita za Saudia katika mikusanyiko ya harusi na misiba.../