Muhammad Abdulsalam: Jamii ya kimataifa inawashajiisha Wasaudia kutenda jinai
Msemaji wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen amelaani jinai zinazoendelea kufanywa na muungano vamizi wa Saudia dhidi ya raia wasio na hatia wala ulinzi wa nchi yake.
Muhammad Abdulsalam amekosoa vikali hatua ya jamii ya kimataifa ya kupuuza dhulma na ukandamizaji unaofanywa na muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya wananchi wa Yemen na kueleza kuwa, jamii ya kimataifa inaushajiisha muungano huo vamizi kutenda jinai zaidi huku ikifumbia macho kikamilifu jinai na dhulma za uvamizi wa nchi ajinabi dhidi ya watu wa Yemen.
Msemaji wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen amesisitiza kuwa kitendo cha jamii ya kimataifa cha kupuuza uhasama wa muungano vamizi wa Saudia na washirika wake ni sawa kabisa na kuushajiisha muungano huo kutenda jinai zaidi dhidi ya Wayemeni na kuzidisha mzingiro wa pande zote kwa nchi hiyo.
Muhammad Abdulsalam ameutaja msimamo wa jamii ya kimataifa mkabala wa muungano vamizi wa Saudia huko Yemen kuwa wa kindumakuwili na kueleza kuwa, hakuna shaka kwamba hatua hizo za undumakuwili zitawazidishia ari na irada wananchi wa Yemen katika kuilinda na kuitetea nchi yao dhidi ya nchi vamizi.