Iraq yatangaza kumalizika majukumu ya wanajeshi wa muungano wa kimataifa
Serikali ya Iraq imetangaza kumalizika rasmi majukumu na kazi za wanajeshi wa eti muungano wa kimataifa chini ya uongozi wa Marekani nchini humo.
Qassim al A'raji Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Iraq ambaye ni mmoja kati ya viongozi wa ngazi ya juu wa nchi hiyo jana Alkhamisi alitangaza kumalizika rasmi majukumu na uwepo wa wanajeshi wa muungano wa kimataifa unaoongozwa na Marekani nchini humo. Al A'raji ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: Leo katika duru ya mwisho ya mazungumzo na viongozi wa ngazi ya juu wa muungano huo wa kimataifa ambayo yalianza mwaka jana, tumetangaza kumalizika rasmi majukumu ya wanajeshi wa muungano huo na vilevile ulazima wa kuondoka vikosi hivyo katika ardhi ya Iraq.
Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Iraq ameongeza kuwa tutaendelea kushirikiana na kuwasiliana na muungano huo wa kimataifa katika masuala ya elimu, kujijengea uwezo na ushauri.
Jumamosi iliyopita Waziri Mkuu wa Iraq Mustafa al Kadhimi na Balozi wa Marekani huko Baghdad, Matthew H. Tueller walifanya mazungumzo kuhusu suala la kuondoka wanajeshi wa Marekani nchini humo.
Viongozi wa Washington awali walikuwa wametangaza kuwa wanajeshi wa Marekani wataondoka katika ardhi ya Iraq ifikapo tarehe 31 Disemba mwaka huu. Mwishoni mwa mwezi wa Kiirani wa Aban mwaka huu viongozi wa Marekani walidai kuwa serikali ya Baghdad inataka kuongezwa muda na kubakia Iraq wanajeshi wake. Baada ya kutolewa maoni hayo, Kamandi ya Oparesheni za Pamoja ya Jeshi la Iraq ilitoa taarifa na kukadhibisha suala la kutaka kuongezwa muda wa kuendelea kuwepo wanajeshi wa Marekani nchini Iraq.