Wasaudia wawashambulia kwa ndege mamluki wao wakidhani ni Ansarullah
Jeshi la anga la Saudi Arabia limefanya mashambulizi makali ya ndege dhidi ya mamluki wake katika mkoa wa Ma'rib nchini Yemen likidhani ni wanamapambano wa ukombozi wa Yemen, Ansarullah.
Tovuti ya "al Khabar al Yamani" imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, ndege moja ya jeshi la anga la Saudi Arabia imeshambulia mkusanyiko wa wanamgambo wa serikali iliyojiuzulu ya Mansour Hadi katika eneo la Wadi Ubaidah mkoani Ma'rib na kuangamiza mamluki kadhaa na kujeruhi wengine wengi.
Wadi Ubaidah ni eneo lililoko kusini mwa mkoa wa Ma'rib. Katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita, eneo hilo limeshuhudia mapigano makali baina ya jeshi na vikosi vya ukombozi vya kujitolea vya wananchi wa Yemen kwa upande mmoja na magaidi wa al Qaida wanaoungwa mkono na Saudi Arabia kwa upande wa pili. Mapema leo alfajiri, jeshi la Yemen limefanikiwa kuteka kambi muhimu zaidi na kubwa zaidi ya magaidi wa al Qaida katika eneo hilo.
Wavamizi wa Kisaudi wanatumia mashambulio ya anga kujaribu kuzuia kusonga mbele jeshi na kamati za kujitolea za wananchi wa Yemen na ni kwa sababu hiyo ndio maana ndege za wavamizi hao zimeshadidisha mashambulizi katika mkoa wa Ma'rib kwa kuona umekaribia kukombolewa na wanamuqawama wa Yemen.
Tarehe 5 mwezi uliopita wa Novemba pia, ndege moja ya Saudi Arabia ilishambulia kimakosa mamluki wake katika eneo la al Falaj la kusini mwa mkoa huo wa Ma'rib na kuua makumi ya mamluki wake na kujeruhi wengine wengi.
Baadhi ya vyombo vya habari vya wavamizi wa Yemen vinasema kuwa, tangu alipoingia madarakani Joe Biden huko Marekani, Washington haiipi Saudia taarifa za kijasusi za medani za vita huko Yemen na ndio maana Saudi Arabia inashambulia mara kwa mara mamluki wake bila ya kukusudia.