Iraq yasisitiza kulindwa umoja wa ardhi yote ya Syria
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq amesema kuwa Baghdad ikiwa kama mwanachama mtazamaji katika kikao cha Astana inasisitiza kuhusu msimamo wake thabiti wa kuunga mkono kupatiwa ufumbuzi mgogoro wa Syria kwa njia za kisiasa.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq jana usiku ilitangaza kuwa, Abdulrahman al Husseini Balozi wa Baghdad mjini Moscow Russia anashiriki katika kikao cha 17 cha Astana katika mji wa Nur -Sultan huko Kazakhstan.
Ahmad al Sahaf Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq ameashiria ushiriki wa nchi hiyo kama mwanachama mtazamaji katika kikao hicho na kueleza kuwa: Al Husseini atakuwa na mazungumzo na jumbe kutoka Syria, Jordan, Lebanon, Russia, Iran, Uturuki na Umoja wa Mataifa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq ameongeza kuwa, Balozi wa Baghdad mjini Moscow amesisitiza kuhusu msimamo imara wa Iraq wa kuunga mkono kupatiwa ufumbuzi mgogoro wa Syria kwa njia za kisiasa.
Kikao cha 17 cha Astana kuhusu Syria kinafanyika katika mji mkuu wa Kazakhstan Nur -Sultan; ambapo jumbe kutoka Iran, Russia, Syria, Uturuki, wapinzani wa Syria, Lebanon na Iraq zinashiriki katika kikao hicho.