Muungano vamizi wa Saudia waendelea kuushambulia mji mkuu wa Yemen, Sana'a
Ndege za muungano vamizi huko Yemen unaoongozwa na Saudi Arabia jana usiku kwa mara nyingine tena ziliushambulia kwa mabomu mji mkuu wa nchi hiyo, Sana'a.
Shirika la habari la Tasnim limearifu kuwa, sauti kubwa za milipuko zilisika jana usiku katika mji mkuu huo wa Yemen. Hadi tunaingia mitamboni hakukuwa na taarifa yoyote kuhusu hasara na maafa yaliyosababishwa na mashambulizi hayo. Ripoti zinasema kuwa ndege za kivita za muungano vamizi zimeendelea kuruka katika anga ya mji mkuu Sana'a.
Muungano huo vamizi wa Saudia katika wiki za karibuni umeshadidisha hujuma na mashambulizi yake dhidi ya maeneo ya raia katika mikoa mbalimbali ya Yemen.
Ikitumia kisingizio cha kutaka kumrejesha madarakani kibaraka wake Abd Rabbuh Mansur Hadi rais mtoro aliyekimbilia Riyadh, tarehe 26 Machi 2015, Saudi Arabia ilianzisha mashambulio makali dhidi ya Yemen, nchi masikini zaidi ya Kiarabu, kupitia muungano wa kijeshi wa nchi kadhaa za Kiarabu na kwa msaada na baraka kamili za Marekani.
Mashambulio hayo yameshaua maelfu ya watu na kuwajeruhi maelfu ya wengine, mbali na mamilioni waliolazimika kuwa wakimbizi. Si hayo tu, bali uvamizi wa Saudia na washirika wake dhidi ya watu wa Yemen umeharibu zaidi ya asilimai 85 ya miundomsingi ya nchi hiyo na kuiacha ikikabiliwa na uhaba mkubwa wa dawa za matibabu na chakula.