Al Haddadi: Marekani inatumia mauzo ya silaha kwa malengo ya kisiasa
Mwanachama wa Muungano wa Utawala wa Sheria wa Iraq amesema Marekani inatumia vibaya silaha za kijeshi kwa malengo yake ya kisiasa.
Alaa al-Haddadi, mjumbe wa Muungano wa Utawala wa Sheria wa Iraq, alisema jana Jumapili kwamba kulikuwepo uwezekano wa kuliangamiza kikamilifu kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) nchini Iraq kwa haraka zaidi, lakini uingiliaji kati wa Marekani ulizuia suala hilo.
Al-Haddadi amesisitiza kuwa, Marekani wakati huo ilikataa kuikabidhi Iraq ndege za kivita za F-16, ikitanguliza maslahi yake kuliko yale ya Iraq, na kwamba kwa sababu hiyo vita dhidi ya Daesh vilichukua miaka kadhaa ili kutimiza malengo ya kisiasa ya Marekani.
Ameongeza kuwa, Marekani ilitumia fursa ya kuendelea kuwepo kwa ISIS ili kuivamia na kuikalia tena Iraq.
Mwanachama huyo wa Muungano wa Utawala wa Sheria amesema kuwa ndege za kivita za F-16 zingeweza kufunga kabisa faili la kundi la kigaidi la ISIS haraka sana, lakini mpango wa Marekani ulikuwa kupeleka tena vikosi vyake nchini Iraq kwa kutumia kisingizio cha kupambana na ugaidi.
Iraqi ilitangaza ushindi dhidi ya kundi la kigaidi la kigaidi la ISIS mwaka 2017 baada ya vita vya miaka mitatu. Hata hivyo mabaki ya wapiganaji wa kundi hilo waliotawanyika huku na kule bado yanafanya hujuma na mashambulizi ya kushtukiza katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Diyala, Kirkuk, Ninawa, Salah al-Din, Al- Anbar na Baghdad.
Kundi la kigaidi la Daesh liliangamizwa nchini Iraq kwa msaada wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran chini ya uongozi wa Kamanda Luteni Jenerali Qasem Soleimani.