Daesh yamchinja askari polisi wa Iraq; al Kadhimi asema watalipiza kisasi
Waziri Mkuu wa Iraq amesema kuwa atalipiza kisasi baada ya kusambaa mkanda mpya wa video uliorushwa hewani na kundi la kigaidi la Daesh ambapo askari polisi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iraq anaonekana akikatwa kichwa na gaidi wa Daesh (ISIS).
Duru za habari zimearifu kuwa, Yasir al - Jourani askari polisi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iraq ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Kitengo cha Pasi za Kusafiria cha al Adhamiyah alikatwa kichwa na Daesh baada ya kutekwa nyara akiwa na wenzake watatu, wakati walipokuwa ziarani katika mkoa wa Diyala.
Msemaji wa Kamandi ya Vikosi vya Ulinzi vya Iraq Yahya Rasoul pia ametoa taarifa akielezea masikitiko yake na kusema kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Mustafa al Kadhimi amesema kwamba magaidi waliotenda jinai hiyo watatiwa mbaroni. Waziri Mkuu wa Iraq amesema kuwa watalipiza kisasi cha mauaji hayo. Yahya Rasoul ametilia mkazo tamko la Waziri Mkuu Mustafa al lKadhimi la kufanywa juhudi zaidi za kitelijinsia na kuendeleza mashambulizi ili kuwaangamiza magaidi wa kundi la Daesh.
Iraq ilitangaza kupata ushindi dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh mwishoni mwa mwaka 2017 kufuatia mchango na uongozi wa makamanda Luteni Jenerali Qasem Soleimani aliyekuwa Mkuu wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) na Abu Mahdi al Muhandes aliyekuwa Naibu Mkuu wa kikosi cha kujitolea cha wananchi wa Iraq cha al Hashdu al Shaabi. Karibu theluthi moja ya ardhi ya Iraq ilikuwa ikikaliwa kwa mabavu na kundi la Daesh tangu mwaka 2014.