Syria yazuia mashambulio ya Wazayuni dhidi yake
Vyanzo vya Syria vimeripoti leo alfajiri kwamba mifumo ya ulinzi wa anga ya nchi hiyo imefanikiwa kuzuia mashambulio yaliyofanywa na utawala ghasibu wa Israel kuulenga mji mkuu wa nchi hiyo Damascus.
Katika miaka ya karibuni utawala huo ghasibu umekuwa ukifanya mashambulio ya anga ya mara kwa mara dhidi ya mji huo na maeneo tofauti ya Syria, mashambulio ambayo mengi yamefelishwa na mifumo ya ulinzi wa anga ya jeshi la Syria kabla ya kufanya uharibufu katika maeneo yaliyolengwa.
Kwa mujibu wa televisheni ya al-Mayadeen, mifumo ya ulinzi wa anga ya Syria imefanikiwa kutungua makombora yaliyorushwa na Wazayuni pembeni ya mji wa Damascus kabla ya kutua na kufanya uharibifu katika maeneo yaliyolengwa.
Uvamizi wa Israel nchini Syria unakuja miezi kadhaa baada ya Scott Ritter, mjumbe wa zamani wa Tume ya Utokomezaji Silaha za Maangamizi ya Iraq kuonya kuwa kuendelea mashambulizi ya utwala wa Israel dhidi ya Syria kunaweza kusababisha mzozo wa kikanda.
Utawala wa Kizayuni daima hulenga maeneo ya jeshi na miundombinu ya Syria katika kuwaunga mkono magaidi wanaoendesha mashambulizi kwa lengo la kuiondoa madarakani serikali halali ya Rais Bashar Asad wa nchi hiyo.
Mgogoro wa Syria ulianza mwaka 2011 kufuatia mashambulizi makubwa yaliyoanzishwa na makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Saudi Arabia, Marekani na washirika wao kwa shabaha ya kubadilisha mlingano wa kieneo na kuimarisha nafasi ya utawala wa Kizayuni katika eneo.
Jeshi la Syria likisaidiwa na washauri wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na uungaji mkono wa Russia, limeweza kulishinda kundi la kigaidi la Daesh nchini humo.
Utawala wa Kizayuni una wasiwasi mkubwa kuhusu uwezekano wa kushindwa kabisa magaidi nchini Syria.