Wazayuni wawaponda kwa farasi Wapalestina, HAMAS yataka maandamano makubwa
Waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari wameripoti kuwa, wanajeshi makatili wa Israel wamewakanyaga kwa farasi Wapalestina waliokuwa wanalalamikia jinai za utawala wa Kizayuni mashariki mwa Baitul Muqaddas inayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni utawala wa Kizayuni.
Waandishi wa shirika la habari la AFP wamesema kuwa, wameona wanajeshi wa Israel wakiwapondaponda kwa farasi Wapalestina baada ya kukataa kuondoka barabarani.
Huku hayo yakiripotiwa, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imetoa mwito kwa wapenda haki ndani na nje ya Palestina kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho ya Wiki ya Kimataifa ya Quds.
Katika siku za hivi karibuni, miji mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jodan likiwemo eneo la Sheikh Jarrah imekumbwa na mapigano baina ya wananchi wa Palestina kwa upande mmoja na wanajeshi na walowezi wa Kizayuni kwa upande wa pili kiasi kwamba baadhi ya wataalamu wa mambo wanasema kuwa, hiyo ni Intifadha mpya imeanza dhidi ya utawala katili wa Kizayuni.
Jana (Jumamosi) harakati ya HAMAS ilitoa taarifa na kutangaza ubunifu wa Wiki ya Kimataifa ya Quds kutokana na Kibla hicho cha Kwanza cha Waislamu kuwa kituo kikuu cha mapambano ya haki dhidi ya batili.
Katika taarifa yake hiyo, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imewataka walimwengu wenye hisia za utu na ubinadamu na vile vile wananchi wa nchi za Kiarabu na Kiislamu, maulamaa na watu wenye ushawishi, vyombo rasmi na visivyo rasmi, vyama vya wananchi na kila asiyependa jinai za Wazayuni, ajitokeze kuadhimisha kwa njia mbalimbali Wiki ya Kimataifa ya Quds yakiwemo maandamano.