Kamanda wa magaidi wa al Qaida aangamizwa Ma'rib nchini Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i81528-kamanda_wa_magaidi_wa_al_qaida_aangamizwa_ma'rib_nchini_yemen
Vyombo mbalimbali vimetangaza habari ya kuangamizwa mmoja wa makamanda wa ngazi za juu wa genge la kigaidi la al Qaida katika mapigano na jeshi la Yemen, mkoani Ma'rib.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 18, 2022 23:17 UTC
  • Kamanda wa magaidi wa al Qaida aangamizwa Ma'rib nchini Yemen

Vyombo mbalimbali vimetangaza habari ya kuangamizwa mmoja wa makamanda wa ngazi za juu wa genge la kigaidi la al Qaida katika mapigano na jeshi la Yemen, mkoani Ma'rib.

Shirika la habari la IRIB limemnukuu kamanda mmoja wa jeshi la Yemen akisema jana Ijumaa kwamba, jeshi la nchi hiyo kwa kushirikiana na vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Yemen linaendelea na mapambano ya ukombozi wa nchi kutoka kwenye makucha ya wavamizi wanaoongozwa na Saudi Arabia na Imarati. Katika mapambano hayo yanayoendelea kwenye maeneo nyeti na muhimu ya mkoa wa Ma'rib, jeshi la Yemen limefanikiwa kuangamiza mamluki na magaidi wengi akiwemo kamanda mmoja wa ngazi za juu wa mtandao wa kigaidi wa al Qaida.

Makundi ya kigaidi likiwemo la al Qaida yamemiminwa katika maeneo ya kusini mwa Yemen na yanafanya kazi kwa usimamiaji kamili wa muungano vamizi unaoongozwa na Saudia na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Mara chungu nzima kumekuwa kukitolewa ushahidi madhubuti usiokanushika wa kushirikiana wavamizi wa Yemen na mgenge ya wakufurishaji ambayo yanatambuliwa kimataifa kuwa ni magenge ya kigaidi.

Vita vya ukombozi wa Ma'rib nchini Yemen

 

Muungano vamizi wa Saudia-Imarati huko Yemen ulianzisha mashambulizi ya kivamizi ya pande zote mwezi Machi 2015, yaani zaidi ya miaka saba iliyopita kwa madai ya kumrudisha madarakani rais zamani wa Yemen, Abdu Rabbuh Mansour Hadi aliyejiuzulu mwenyewe na kukimbilia Saudi Arabia. 

Matokeo ya uvamizi huo ni kushuhudiwa jinai kubwa mno dhidi ya wananchi Waislamu wa Yemen na licha ya kupita zaidi ya miaka 7, lakini wavamizi wa nchi hiyo ya Kiarabu wameshindwa kufanikisha malengo yao kutokana na muqawama na mapambano ya kishujaa ya Wayemen.