Marekani yakasirishwa na safari ya Bashar al Assad nchini Imarati
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i81544-marekani_yakasirishwa_na_safari_ya_bashar_al_assad_nchini_imarati
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani amepinga safari iliyofanywa jana Ijumaa na Rais bashar Assad wa Syria nchini Imarati.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 19, 2022 03:42 UTC
  • Marekani yakasirishwa na safari ya Bashar al Assad nchini Imarati

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani amepinga safari iliyofanywa jana Ijumaa na Rais bashar Assad wa Syria nchini Imarati.

Ziara ya Rais wa Syria Bashar al-Assad katika UAE inakuja kinyume na matakwa ya Washington, ambapo nchi za Kiarabu waitifaki wa Marekani ambazo hapo awali zilikuwa katika kambi moja ya kuiangusha serikali halali ya Syria, sasa zimebadili mwelekeo na misimamo yao ya hapo awali na kuanza kuhuisha uhusiano wao wa kidiplomasia na kiuchumi na serikali ya Bashar al Assad. 

Televisheni ya Al-Jazeera ya Qatar imemnukuu msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani akisema: "Tunasikitishwa na juhudi za kuhalalisha utawala wa Bashar al-Assad."

Mwanadiplomasia huyo wa Marekani pia amedai kuwa Bashar al-Assad amehusika na vifo na mateso ya idadi kubwa ya Wasyria, hivyo wale wanaofikiria kushirikiana na utawala wa Assad wanapaswa kuzingatia uhalifu wake.

Msimamo huo wa wazi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani dhidi ya kurejeshwa uhusiano wa kawaida baina ya nchi za Kiarabu na Syria unaonyesha kuwa serikali ya Joe Biden, kama zilivyokuwa tawala zilizopita za Marekani, inataka kupinduliwa serikali halali ya Syria na hivyo inapinga hatua yoyote ya kuitambua au kuiimarisha serikali hiyo.

Katika ziara yake ya Ijumaa ya jana huko UAE, Bashar al-Assad alikutana na maafisa kadhaa wa Imarati, akiwemo mtawala wa Dubai, Mohammed bin Rashid Al Maktoum na Mwanamfalme wa Abu Dhabi Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan.

Bashar Assad na Mwanamfalme wa Abu Dhabi Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan

Syria imekuwa uwanja wa mapigano makali tangu mwaka 2011 kati ya vikosi vya jeshi la serikali ya nchi hiyo na makundi ya kigaidi na kitakfiri.

Ripoti nyingi zikiwemo za vyombo vya habari vya Magharibi, zinaonyesha kuwa nchi za Magharibi zimetoa msaada wa silaha, ujasusi na silaha kwa makundi hayo ili kuiangusha serikali ya Syria.

Serikali ya Bashar Al Assad daima imekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya utawala haramu wa Israel na katika kuwatetea watu wanaodhulumiwa wa Palestina.