Yemen yafanya mashambulizi kadhaa ya kulipiza kisasi ndani ya Saudi Arabia
Vikosi vya Jeshi la Yemen, vikisaidiwa na wapiganaji wa harakati ya wananchi ya Ansarullahu, vimeanzisha mashambulizi mapya ya kulipiza kisasi dhidi ya Saudi Arabia, ikiwa ni pamoja na hujuma iliyolenga kituo kinachoendeshwa na kampuni ya mafuta ya Aramco katika eneo la kistratijia la Jizan, ili kulipiza kisasi uchokozi wa kijeshi za utawala wa Riyadh dhidi ya raia wasio na hatia wa Yemen.
Ni baada ya shirika rasmi la habari la Saudi Arabia, likinukuu taarifa ya muungano unaoongozwa na Riyadh, kutangaza mapema leo Jumapili kwamba mashambulizi hayo ya Jeshi la Yemen yamelenga kiwanda cha kusafisha maji katika mji wa al-Shaqeeq, kituo cha shirika la mafuta la Aramco huko Jizan, kituo cha nguvu za umeme kusini mwa Dhahran al- Janub, na kituo cha gesi huko Khamis Mushait.
Msemaji wa jeshi la Yemen baadaye alithibitisha mashambulizi hayo, akisema jeshi hilo limefanya mashambulizi makubwa yaliyopewa jina la Operesheni ya Kuvunja Mzingiro-2, dhidi ya malengo kadhaa muhimu na nyeti ndani ya Saudi Arabia, kwa kutumia makombora ya balestiki na ndege zisizo na rubani.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari katika mji mkuu wa Yemen, Sana'a leo Jumapili, Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema wanajeshi wa Yemen na washirika wao wameshambulia vituo vya kampuni ya Aramco katika mji mkuu wa Saudia, Riyadh, mbali na maeneo kadhaa muhimu katika miji ya Yanbu, Abha, Khamis Mushait, Jizan, Samtah na Dhahran al-Janub.
Brigedia Jenerali Yahya Saree ameongeza kuwa: “Mungu akipenda, vikosi vya jeshi vya Yemen vitaendelea na operesheni maalumu za kijeshi ili kuvunja mzingiro wa kikatili. Mashambulizi hayo yatalenga maeneo muhimu na nyeti, ambayo adui hawezi kamwe kufikiria."
Amesema Jeshi la Yemen linamuonya adui mtenda jinai kuhusu matokeo ya mzingiro wake wa kidhalimu dhidi ya watu wa Yemen na kwamba vikosi vya jeshi hilo vitaendelea kushambulia vituo vya kimkakati na nyeti vya nchi wanachama wa muungano unaoongozwa na Saudi Arabia hadi nchi hizo zitakapokomesha mzingiro huo.
Saudi Arabia, ikiongoza muungano wa nchi kadhaa zinazosaidiwa na Marekani, Uingereza na utawala haramu wa Israel, imekuwa ikifanya uvamizi wa kijeshi na kuizingira Yemen kutokea pande zote za nchi kavu, anga na baharini tangu Machi 2015.