Saree: Tutaendeleza mashambulizi mapya dhidi ya Saudia hadi tuvunje mzingiro
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i81656-saree_tutaendeleza_mashambulizi_mapya_dhidi_ya_saudia_hadi_tuvunje_mzingiro
Msemaji wa Jeshi la Yemen amesema vikosi vya jeshi hilo vitaendelea kushambulia vituo vya kimkakati na nyeti vya nchi wanachama wa muungano unaoongozwa na Saudi Arabia katika mashambulizi makubwa yaliyopewa jina la Operesheni ya Kuvunja Mzingiro, hadi nchi hizo zitakapokomesha mzingiro huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 22, 2022 01:59 UTC
  • Saree: Tutaendeleza mashambulizi mapya dhidi ya Saudia hadi tuvunje mzingiro

Msemaji wa Jeshi la Yemen amesema vikosi vya jeshi hilo vitaendelea kushambulia vituo vya kimkakati na nyeti vya nchi wanachama wa muungano unaoongozwa na Saudi Arabia katika mashambulizi makubwa yaliyopewa jina la Operesheni ya Kuvunja Mzingiro, hadi nchi hizo zitakapokomesha mzingiro huo.

Brigedia Jenerali Yahya Saree alisema hayo jana Jumatatu katika kikao na waandishi wa habari mjini Sanaa na kuongeza kuwa, vikosi vya jeshi vya Yemen vikisaidiwa na wapiganaji wa harakati ya wananchi ya Ansarullah vitaendelea na operesheni maalumu za kijeshi kwa shabaha ya kulipiza kisasi na kuvunja mzingiro huo wa kikatili.

Ameeleza bayana kuwa, licha ya mzingiro wa kila upande na hujuma za kila aina za wavamizi tangu tangu Machi 2015, lakini wananchi wa Yemen wamesimama kidete mkabala wa uvamizi na mzingiro wa Saudia na waitifaki wake.

Msemaji wa Jeshi la Yemen ameongeza kuwa, vikosi vya Yemen vimeangamiza wapiganaji 20,000 wa muungano vamizi wa Saudi Arabia, wakiwemo askari 10,000 wa Kisaudi na 1,200 wa Imarati. 

Shambulio dhidi ya shirika la mafuta la Aramco la Saudia

Kauli ya Jenerali Saree imekuja wakati huu ambapo mashambulizi ya makombora ya balestiki na ndege zisizo na rubani za jeshi la Yemen na wapiganaji wa harakati ya Ansarullah dhidi ya maeneo ya ndani kabisa ya Saudia yamechachamaa.

Hivi karibuni, wanajeshi wa Yemen na washirika wao walishambulia vituo vya kampuni ya Aramco katika mji mkuu wa Saudia, Riyadh, mbali na maeneo kadhaa muhimu katika miji ya Yanbu, Abha, Khamis Mushait, Jizan, Samtah na Dhahran al-Janub.