Saudia yakimbilia kwa UN kuomba kukwamuliwa kutoka kwenye kinamasi cha Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i81814-saudia_yakimbilia_kwa_un_kuomba_kukwamuliwa_kutoka_kwenye_kinamasi_cha_yemen
Baada ya jeshi la Yemen kutoa pigo jingine kubwa la mashambulio ya makombora ndani ya ardhi ya Saudi Arabia, sasa viongozi wa ukoo wa Aal Saud wamekimbilia kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuomba kusaidiwa kutoka katika kinamasi cha Yemen walichojitumbukiza mwezi Machi, 2015.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Mar 26, 2022 09:19 UTC
  • Saudia yakimbilia kwa UN kuomba kukwamuliwa kutoka kwenye kinamasi cha Yemen

Baada ya jeshi la Yemen kutoa pigo jingine kubwa la mashambulio ya makombora ndani ya ardhi ya Saudi Arabia, sasa viongozi wa ukoo wa Aal Saud wamekimbilia kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuomba kusaidiwa kutoka katika kinamasi cha Yemen walichojitumbukiza mwezi Machi, 2015.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, Saudi Arabia imeomba kuitishwa kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa cha kulaani mashambulizi makubwa yaliyofanywa na majeshi ya Yemen ndani ya ardhi ya Saudia, kwa ajili ya kulipiza kisasi jinai zisizo na kifani za wavamizi wa Yemen.

Ofisi ya mwakilishi wa kudumu wa Saudi Arabia katika Umoja wa Mataifa imeliandikia barua Baraza la Usalama la umoja huo na kuliomba lilaani mashambulio hayo dhidi ya miundombinu nyeti na muhimu sana ya Saudia.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

 

Ofisi ya kudumu ya Saudia katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini Washington Marekani imetumia ukurasa wake wa Twitter  na kusema, mashambulio ya mara kwa mara ya jeshi la Yemen kwenye taasisi za mafuta za nchi hiyo likiwemo shambulia la jana Ijumaa, tarehe 25 Machi, 2022 na pia shambulizi dhidi ya taasisi ya mafuta ya al Mukhtar huko Jizan, ni tishio kwa usalama wa dunia nzima. 

Hii ni katika hali ambayo, Waziri wa Habari wa Yemen Zaifullah al-Shami ameiambia Saudi Arabia kwamba: "Moto unaowaka huko Aramco ni matunda ya jinai za Saudia na kuendelea kuzingirwa watu wa Yemen, na hakuna serikali itakayoweza kuuzima moto huo hadi mzingiro wa Yemen utakapoondolewa."

Kwa upande wake, Msemaji wa Jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree, amesema, vikosi vya jeshi hilo vitaendelea kushambulia vituo vya kimkakati na nyeti vya nchi wanachama wa muungano vamizi unaoongozwa na Saudia, hadi nchi hizo zitakapokomesha mzingiro huo.