Hizbullah: Hatutasalimu amri kwa uvamizi wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i81828-hizbullah_hatutasalimu_amri_kwa_uvamizi_wa_israel
Naibu Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa harakati hiyo haikubali kwa gharama yoyote vitendo vya kughusubu na ukaliaji mabavu wa Israel, na wala haitasalimu amri mbele ya njama za Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 27, 2022 03:10 UTC
  • Hizbullah: Hatutasalimu amri kwa uvamizi wa Israel

Naibu Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa harakati hiyo haikubali kwa gharama yoyote vitendo vya kughusubu na ukaliaji mabavu wa Israel, na wala haitasalimu amri mbele ya njama za Marekani.

Marekani na waitifaki wake kwa miaka kadhaa sasa haziachi kufanya njama dhidi ya wananchi wa Lebanon na kila uchao pande hizo za Magharibi zinapanga na kutekeleza njama mpya dhidi ya nchi hiyo. Wananchi wa Lebanon kwa zaidi ya miaka miwili sasa wanataabika na hali mbaya ya uchumi ikiwa ni matokeo ya njama za Marekani, Wazayuni, Saudia na vibaraka wao wa ndani.  

Sheik Naim Qassim, Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa: Hizbullah siku zote inaliunga mkono na kulisaidia jeshi la Lebanon na haijawahi kusema kuwa itachukua nafasi ya jeshi, bali jeshi lenyewe linapasa kutekeleza majukumu yake ya kuilinda Lebanon na kukomboa ardhi za nchi hiyo.   

Sheikh Qassim ameashiria mafanikio ya muqawama katika kukomboa ardhi ya Lebanon, kushindwa utawala haramu wa Israel na kuangamizwa matakfiri na kueleza kuwa: silaha ya muqawama imeyakomboa maeneo ya kusini na eneo la al Bekaa huko magharibi mwa Lebanon na kuyafuruisha makundi ya Daesh na Jabhatul Nusra. Si hayo tu bali silaha ya muqawama imeleta mlingano katika kukabiliana na mashambulizi na hujuma huko Lebanon. 

Nabih Berri Spika wa Bunge la Lebanon huko nyuma aliwahi kusema kuwa, muqawama wa Lebanon (Hizbullah) ndio nguvu ya kuihami nchi hiyo sambamba na kuendesha mapambano ya kisiasa ya kuainisha mipaka na haki ya kujitawala katika mipaka ya majini na nchi kavu.   

Nabih Berri, Spika wa Bunge la Lebanon