Mahmoud Abbas asisitiza kutekelezwa mpango wa 'amani' wa Ufaransa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i8365-mahmoud_abbas_asisitiza_kutekelezwa_mpango_wa_'amani'_wa_ufaransa
Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesisitiza tena kutekelezwa mpango wa Ufaransa wa kutatua kadhia ya Palestina licha ya Wapalestina wenyewe kuupinga mpango huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 03, 2016 02:52 UTC
  • Mahmoud Abbas asisitiza kutekelezwa mpango wa 'amani' wa Ufaransa

Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesisitiza tena kutekelezwa mpango wa Ufaransa wa kutatua kadhia ya Palestina licha ya Wapalestina wenyewe kuupinga mpango huo.

Abbas ametoa sisitizo hilo Ramallah, Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland, Timo Soini na kuitaka Jamii ya Kimataifa iunge mkono mpango wa Ufaransa wa kufanyika mkutano wa kimataifa wa Paris kwa lengo la kutatua kadhia ya Palestina.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland amesema, nchi yake inaunga mkono kutatuliwa suala la Palestina kwa msingi wa kuundwa nchi huru ya Palestina.

Katika mazungumzo hayo, pande hizo mbili zimesisitiza juu ya kuendelezwa juhudi za kimataifa kwa lengo la kufanikisha mazungumzo kwa msingi wa kuundwa nchi huru ya Palestina kulingana na mipaka ya mwaka 1967.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland amekutana na kufanya mazungumzo pia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina Riyadh al-Maliki.

Katika mazungumzo hayo, al- Maliki amesema utawala wa Kizayuni una hofu na mkutano wa kimataifa wa Paris uliopangwa kuanza leo katika mji mkuu huo wa Ufaransa. Ifahamike kuwa licha ya mpango eti wa 'amani' wa Ufaransa kukidhi maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel, lakini utawala huo umeukataa mpango huo.../