Syria: UN inatia siasa kwenye masuala ya kibinadamu nchini humo
Balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa amekosoa hatua ya Baraza la Usalama la umoja huo kutia kile alichokitaja kuwa siasa kuhusu hali ya kibinadamu katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Bashar al-Jaafari, Mwakilishi wa kudumu wa Syria katika Umoja wa Mataifa amesema lengo la baadhi ya nchi wanachama wa Baraza la Usalama la umoja huo ni kuishinikiza serikali halali ya Rais Bashar al-Assad kujiuzulu, badala ya kupambana na magenge ya kigaidi. Akiongea jana Ijumaa na shirika rasmi la habari la Syria SANA, al-Jaafari alisema na hapa tunamnukuu: "Dhamira ya baadhi ya nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni kuingilia masuala ya ndani na uhuru wa kujitawala wa Syria na kufumbia macho juhudi za serikali ya Damascus za kukabiliana na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh."
Wakati huo huo, Mwakilishi wa kudumu wa Syria katika Umoja wa Mataifa amepuuzilia mbali madai ya kipropaganda yanayoenezwa na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi, kwamba eti serikali ya Assad imezuia kupelekwa misaada ya kibinadamu katika maeneo ambayo yanadhibitiwa na makundi ya kigaidi huku akisisitiza kuwa, Syria inashirikiana kwa kila hali na Umoja wa Mataifa, Shirika la Hilali Nyekundu na mashiriki mengine ya kibinadamu kuhakikisha kuwa misaada hiyo ya kibinadamu inawafikia wananchi bila ubaguzi wa aina yeyote.
Mgogoro wa Syria ulinza mwaka 2011 baada ya magenge ya kitakfiri yanayoungwa mkono na madola ya kigeni kuivamia nchi hiyo kwa uungaji mkono wa Marekani na waitifaki wake kwa nia ya kuipundua serikali ya Rais Bashar al-Assad iliyoko madarakani kwa ridhaa ya wananchi.