Serikali ya Taliban nchini Afghanistan mbioni kustawisha uhusiano mwema na majirani
Amir Khan Motaqi, Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa serikali ya Taliban nchini Afghanistan amesema kuwa, njia za mpakani za nchi hiyo ziko wazi kwa ajili ya majirani na kwamba, serikali ya Taliban ina uhusiano mwema na mzuri na majirani zake.
Amir Khan Motaqi ameongeza kuwa, sera za kigeni za kundi la Taliban linalotawala nchini Afghanistan ni kuwa na uhusiano wenye uwiano na mataifa jirani na kwamba, hakuna tatizo au kikwazo juu ya kuwa na uhusiano wa kidiplomasia au kibiashara na mataifa mengine.
Matamshi ya Amir Khan Motaqi, Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa serikali ya Taliban nchini Afghanistan yanatolewa katika hali ambayo, baada ya kupita miezi 10 tangu Taliban itwae hatamu za uongozi nchini Afghanistan, hadi sasa hakuna nchi yoyote ambayo imelitambua rasmi kundi hilo na kwa mujibu wa vigezo vya kimataifa vya ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi kundi la Taliban halina uhalali kimataifa.
Kundi la Taliban ambalo lilitwaa madaraka nchini Afghanistan Agosti mwaka jana (2021), hivi sasa limo mbioni kupanua na kustawisha uhusiano na mataifa jirani na ya nje ya eneo hili.
Juhudi za serikali ya Taliban nchini Afghanistan za kupanua ushirikiano na mataifa jirani ni ishara ya wazi ya hitajio la serikali hiyo kwa mahusiano na mataifa ya jirani.
Kuhusiana na suala hilo, Fereydoon Barkazi mweledi na mtaalamu wa masuala ya Afghanistan ameziambia duru za habari kwamba, serikali ya Taliban inapaswa kupata ibra na funzo kupitia matukio ya huko nyuma na ijiepushe na kutekeleza sheria zilizokuwa zikitekelezwa na uongozi wa utawala wake huko nyuma hatua ambazo zilipelekea kutotambuliwa rasmi na jamii ya kimataifa.
Kudhaminiwa haki za kimsingi za wanawake na kufunguliwa kikamilifu shule za wasichana, kutotumiwa ardhi ya Afghanistan dhidi ya mataifa mengine na kuundwa serikali jumuishi nchini Afghanistan ni miongoni mwa masharti ya jamii ya kimataifa kwa ajili ya kuitambua rasmi serikali ya Taliban.
Katika miezi ya hivi karibuni, majirani wa Afghanistan ikiwemo Tajikistan na Uzbekistan wameshambuliwa kutoka ndani ya Afghanistan ambapo kundi la kigaidi la Daesh limetangaza kuhusika na hujuma na mashambulio hayo.
Mashambulio hayo ya makombora kutoka ndani ya ardhi ya Afghanistan na kulenga mataifa jirani, yamefanyika katika hali ambayo, serikali ya muda ya Afghanistan imetangaza kuwa, ardhi ya nchi hiyo siyo tishio kwa mataifa jirani na kulipuuza kundi la Daesh.
Juhudi hizi za serikali ya wanamgambo wa Taliban za kupanua ushirikiano na majirani zina umuhimu wa pande kadhaa.
Mosi, kwa hatua hii, serikali ya Taliban inataka itambuliwe rasmi na mataifa jirani na kisha baadaye nje ya eneo na kimataifa.
Pili ni kuwa, serikali ya Taliban inayahitajia mataifa jirani ili iweze kukabiliana na matatizo ya kiuchumi na mgogoro wa kibinadamu ambao chimbuko lake ni kukaliwa kwa mabavu.
Gholam Sakhi Ehsani, mweledi wa Kiafghani amesema katika mahojiano aliyofanyiwa na Shirika la Habari la Shafaqna kwamba: Filihali umasikini na ukosefu wa ajira vinazidi kuongezeka huku harakati za shughuli za kiuchumi na sekta ya uzalishaji vikielekea kusimama kikamilifu.
Hivi sasa inaonekana kuwa, serikali ya Taliban imefahamu kwamba, inaweza kuyapatia ufumbuzi matatizo inayokabiliwa nayo kwa kutegemea uwezo wa ndani na kwa kupanua ushirikiano na uhusiano na mataifa jirani, matatizo ambayo yametokana na uwepo wa miaka kadhaa wa vikosi vya kigeni vikiwemo vya Marekani katika nchi hiyo.
Vikosi vya Marekani vilikuwa nchini Afghanistan kwa muda wa miaka 20 ambapo Washington kupitia uwepo wa jeshi lake, ilikusudia kufikia malengo yake katika eneo la Asia Magharibi. Hata hivyo, Agosti mwaka jana (2021) Marekani ililazimika kuondoa majeshi yake baada ya kushindwa kufikia malengo yake. Uwepo wa miongo miwili wa Marekani nchini Afghanistan umepelekea kusambaratika kabisa miundomsingi ya kiuchumi na sekta nyingine nchini humo.
Kwa muktadha huo, serikali ya Taliban kwa kupanua uhusiano na majirani zake ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Pakistan ambazo zimekuwa zikitangaza daima utayari wa kushirikiana na serikali ya Kabul, kunaleta matumaini ya kupatikana mustakabali mwema pasi na kuweko majeshi ya kigeni. Uhusiano na ushirikiano ambao utakuwa ni kwa maslahi na manufaa ya Afghanistan na wananchi wa nchi hiyo.