IMF: Theluthi moja ya wananchi wa Yemen hawana usalama wa chakula
Shirika la Fedha Duniani (IMF) limetangaza kuwa, theluthi moja ya wananchi wa Yemen hawana usalama wa chakula kutokana na kuongeza kimataifa bei za bidhaa za chakula.
Taarifa iliyotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) imebainisha kwamba, kuongezeka kwa bei za bidhaa za chakula, mgogoro wa kiuchumi na kibinadamu kumeifanya hali ya mambo katika nchi ya Yemen kuzidi kuwa mbaya hasa katika sekta ya chakula.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, theluthi moja ya wananchi wa Yemen wanataabika hivi sasa kutokana na kuongezeka kwa bei za chakula na hivyo kuwafanya wakabiliwe na ukosefu wa usalama wa chakula.
Hivi karibuni pia, Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) ulitangaza kuwa, mamilioni ya watoto wa Yemen wapo katika hatari ya kupoteza maisha kutokana na kuandamwa na njaa, huku muungano wa kivita unaoongozwa na Saudi Arabia ukiendelea kufanya mashambulizi na kuliwekea mzingiro wa kila upande taifa hilo maskini la Kiarabu.
Ripoti rasmi zinaonesha kuwa, watoto 300 wa Yemen wanafariki dunia ndani ya kila saa 24 kutokana na utapiamlo wa kiwango cha juu.
Wakati huuo huo, kundi la kukabiliana na migogoro ya chakula na nishati lenye mfungano na Umoja wa Mataifa limetangaza kuwa, baada ya kupita miezi mitatu tangu kuanza vita vya Russia na Ukraine, ulimwengu unakabiliwa na tatizo la chakula linaloongezeka kila siku ambalo limeathiri maisha ya watu bilioni 1.6 kote ulimwenguni.