Syria: Vikwazo vya UN viondolewe, Marekani na Uturuki zikomeshe uvamizi
Serikali ya Syria, kwa mara nyingine tena, imetoa wito wa kuondolewa mara moja na bila ya masharti vikwazo vya upande mmoja na kuondoka vikosi vamizi vya askari wa Marekani na Uturuki katika ardhi yake.
Mwakilishi wa kudumu wa Syria katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa na mashirika la kimataifa mjini Geneva, Hussam al-Din Ala amesema katika kikao cha Baraza la Haki za Binadamu kwamba Damascus inapinga mazungumzo ya baraza hilo kuhusu Syria na kuongeza kuwa: Mazungumzo hayo yana upendeleo na yanatokana na uingiliaji kati na maamuzi yasiyo sahihi ya Marekani na Umoja wa Ulaya.
Mwakilishi huyo wa Kudumu wa Syria huko Geneva ameeleza kuwa wakati serikali ya Damascus ikiendeleza juhudi za kuimarisha usalama, kuboresha uchumi wa nchi, hali ya maisha ya taifa hilo na kurahisisha mwenendo wa kurejea wakimbizi nchini, Syria inasumbuliwa na uvamizi na kukaliwa kwa mabavu sehemu ya ardhi yake kunakofanywa na Uturuki, Israel na Marekani, kuendelea misaada yao kwa makundi ya kigaidi na waasi wanaotaka kujitenga na uporaji wa mafuta, gesi na ngano ya nchi inayotoroshwa na kuuzwa kwa njia za magendo.
Ala pia ametahadharisha kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanyika katika maeneo ya kaskazini mwa Syria yanayokaliwa kwa mabavu na Uturuki kutokana na sera za utawala wa Ankara za kutaka kubadilisha muundo wa jamii ya eneo hilo na uvamizi wa magaidi mamluki wa serikali ya Uturuki dhidi ya maisha na mali za raia wa Syria.
Mwakilishi wa Syria katika mashirika ya kimataifa amesema vitisho vya Uturuki vya kuanzisha eti "ukanda wa amani" kaskazini mwa Syria vinaendana na njama zenye uharibifu na hujuma za utawala wa Ankara dhidi ya ardhi na watu wa Syria.
Jeshi la Uturuki limevamia na kukalia kwa mabavu maeneo ya kaskazini na kaskazini mashariki mwa Syria kwa muda wa miaka miwili na nusu iliyopita kwa kisingizio cha kupambana na magaidi.