EU yaonya kuhusu Israel kuwatimua Wapalestina Masafer Yatta
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i85634-eu_yaonya_kuhusu_israel_kuwatimua_wapalestina_masafer_yatta
TEHRAN (IQNA) - Mwanadiplomasia mwandamizi wa Umoja wa Ulaya ameelezea wasiwasi wake kuhusu uwezekano wa idadi kubwa ya Wapalestina kuhamishwa kwa nguvu kutoka eneo la mashambani katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan linalokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 08, 2022 23:04 UTC
  • EU yaonya kuhusu Israel kuwatimua Wapalestina Masafer Yatta

TEHRAN (IQNA) - Mwanadiplomasia mwandamizi wa Umoja wa Ulaya ameelezea wasiwasi wake kuhusu uwezekano wa idadi kubwa ya Wapalestina kuhamishwa kwa nguvu kutoka eneo la mashambani katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan linalokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Sven Kuehn von Burgsdorff, balozi wa Umoja wa Ulaya huko Palestina, ameonya kwamba hatua ya utawala wa Kizayuni wa kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina itakuwa ni "uhamisho mkubwa zaidi wa nguvu kwa miongo kadhaa."

Sven Kuehn von Burgsdorff, ametoa tahadhari hiyo baada ya kuzuru eneo la Masafer Yatta kusini mwa Ukingo wa Magharibi, ambapo kufukuzwa kwa Wapalestina kumeongezeka baada ya uamuzi wenye utata wa mahakama ya utawala haramu wa Israel mwezi Mei.

Mahakama kuu ya utawala wa Tel Aviv ilitoa uamuzi tarehe 4 Mei kwamba zaidi ya wakazi 1,000 wa vijiji vya Masafer Yatta "wameshindwa kuthibitisha" madai yao ya makazi ya kudumu katika eneo hilo kabla ya jeshi la Israel kulitangaza kuwa ni eneo maalumu la mazoezi ya kijeshi, ambapo uwepo wa raia ni marufuku.

Von Burgsdorff amesisitiza kwamba kumekuwa na ongezeko kubwa la ubomoaji tangu uamuzi huo, huku chanzo cha Umoja wa Ulaya kikisema kuwa majengo 27 yamebomolewa na angalau maagizo 30 zaidi ya kubomoa yametolewa zaidi ya mara mbili ya kiwango katika miaka ya hivi karibuni.

Bulldoza za utawala wa Kizayuni wa Israel zikibomoa nyumba za Wapalestina

Mwanzoni mwa miaka ya 1980, jeshi la Israel lilitangaza eneo hilo la kilomita 30 za mraba kuwa eneo la kijeshi lililowekewa vikwazo na kudai kuwa halikaliwi na watu huku Wapalestina waliokuwa wakiishi huko wakisema ni makazi ya watu wao muda mrefu kabla ya vikosi vya Israel vinavyolikalia kwa mabavu kukanyaga Ukingo wa Magharibi.

Von Burgsdorff amesema majaji wakuu wa Israel wamepuuza sheria za kimataifa katika hukumu hiyo ambayo "inaonekana kupuuza" majukumu ya utawala huo kwa wakaazi wa Palestina kama "nguvu inayokalia kwa mabavu."

Tayari Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imetangaza kuwa kufukuzwa Wapalestina kutoka eneo la Masafer Yatta, kunaweza kuwa sawa na kuwalazimisha kuyahama makazi yao, jambo ambalo ni ukiukaji mkubwa wa Mkataba wa Nne wa Geneva na hivyo kuzingatiwa kuwa ni uhalifu wa kivita.