HAMAS: Watawala Waarabu waliohadaiwa waangalie upya uamuzi wao
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i85664-hamas_watawala_waarabu_waliohadaiwa_waangalie_upya_uamuzi_wao
Mkuu wa ofisi ya uhusiano na nchi za Kiarabu na Kiislamu ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema, watawala Waarabu waliohadaiwa wakaanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel, waangalie upya uamuzi wao huo waliochukua.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 09, 2022 22:15 UTC
  • HAMAS: Watawala Waarabu waliohadaiwa waangalie upya uamuzi wao

Mkuu wa ofisi ya uhusiano na nchi za Kiarabu na Kiislamu ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema, watawala Waarabu waliohadaiwa wakaanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel, waangalie upya uamuzi wao huo waliochukua.

Kwa mashinikizo ya aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump, hadi sasa nchi nne za Kiarabu, ambazo ni Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE), Bahrain, Sudan na Morocco zimefikia makubaliano rasmi na utawala haramu wa Israel ya kuanzisha uhusiano kamili wa kidiplomasia.

Khalil al Hayyah, Mkuu wa ofisi ya uhusiano na nchi za Kiarabu na Kiislamu ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS ameiambia redio ya Al Aqsa, "watu wanaofanya hima ili kuuweka mbali umma wa Mtume Muhammad SAW na dini yao watashindwa, kwa sababu umma wetu ni mwaminifu kwa Quds na Msikiti wa Aqsa".

Khalil al Hayya

Al Hayyah ameongezea kwa kusema: "Palestina, Quds na Msikiti wa Al Aqsa ni vielelezo vya mapambano dhidi ya maghasibu wa Kiisrael; na sisi tutashinda katika mapambano ya kuupigania msikiti wa Al Aqsa".

Halikadhalika, mkuu huyo wa ofisi ya uhusiano na nchi za Kiarabu na Kiislamu ya HAMAS amesisitiza kuwa, wafanyamapatano walitaka kuipindisha dira ya umma ili msikiti wa Aqsa usibaki kuwa kadhia inayohusisha mapambano dhidi ya maghasibu, lakini msikiti huo umeendelea kubaki kuwa ajenda kuu ya makabiliano na wazayuni; na watu waumini na wenye imani wa mashariki na magharibi ya dunia wanapiga mayowe ya kuinadi Palestina.

Hatua ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala bandia wa Israel imepingwa na nchi nyingi pamoja na watu wengi ulimwenguni.../