Bunge la Syria laanza vikao, lamchagua Spika mwanamke
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i8662-bunge_la_syria_laanza_vikao_lamchagua_spika_mwanamke
Kwa mara ya kwanza kabisa, bunge la Syria limemteua mwanamke kuwa spika mpya wa bunge hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 07, 2016 03:00 UTC
  • Bunge la Syria laanza vikao, lamchagua Spika mwanamke

Kwa mara ya kwanza kabisa, bunge la Syria limemteua mwanamke kuwa spika mpya wa bunge hilo.

Shirika la habari la nchi hiyo SANA limetangaza kuwa, Hadiya al-Abbasi mwenye umri wa miaka 58 alichaguliwa jana kuwa Spika wa bunge la Syria, katika kikao cha kwanza tangu kufanyika uchaguzi wa bunge mwezi Aprili mwaka huu. Al-Abbasi mwenye shahada ya uzamifu (PhD) ya uhandisi wa kilimo anakuwa mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kuwa spika wa bunge la Syria, tangu mwaka 1919.

Kati ya mwaka 1988-1998, Hadiya al-Abbasi alikuwa mwanachama wa Baraza Kuu la chama tawala cha Baath katika mkoa wa Deir ez-Zour na baadaye alichaguliwa kuwa mbunge kati ya mwaka 2003-2007.

Tangu kupasishwa kwa sheria ya kuwaruhusu wanawake kupiga kura na kuwania viti mbali mbali, idadi ya wabunge wa kike katika nchi hiyo ya Kiarabu imekuwa ikiongezeka.

Itakumbukwa kuwa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Syria ilisema kuwa, chama tawala cha Baath cha Rais Bashar al-Assad ambacho kilikuwa chini ya muungano wa Umoja wa Taifa kilishinda viti 200 kati ya 250 vya bunge la nchi hiyo katika uchaguzi wa Aprili 13.