Dec 14, 2022 07:50 UTC
  • Walowezi wa Kizayuni wavamia tena msikiti wa al-Aqswa

Makumi ya walowezi wa Kizayuni wameuvamia tena Msikiti wa al-Aqswa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kuuvunjia heshima msikiti huo mtakatifu.

Ripoti zaidi zinasema kuwa, katika muendelezo wa hujuma na vitendo vya chuki vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina, makumi ya walowezi wa Kiyahudi wamevamia tena msikiti mtakatifu wa al-Aqswa kibla cha kwanza cha Waislamu.

Walowezi hao wa Kizayuni wakisaidiwa na kupewa himaya na jeshi la Israel baada ya kuingia katika eneo la ndani la msikiti huo mtakatifu walisikika wakipiga nara dhidi ya Uislamu na Waislamu na kufanya vitendo vya kuchochea hisia za Waislamu.

Kitengo cha Upashaji Habari cha Palestina katika Idara ya Wakfu za Kiislamu katika mji wa Quds kimetangaza kuwa, makumi ya walowezi wa Kizayuni jana walivamia msikiti wa al-Aqswa kupitai Babul al-Maghariba.

Katika miezi ya hivi karibuni vitendo vya hujuma na uvamizi wa walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina hususan katika Msikiti wa al-Aqswa vimeongezeka mno.

 

Vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za maana za kukabiliana na vitendo hivyo vinavyokinzana na utu na ubinadamu.

Utawala wa Kizayuni ambao unaungwa mkono kikamilifu na Marekani katika hatua zake hizo haramu umedhamiria kubadilisha muundo wa kijiografia na kidemografia wa maeneo ya Palestina; ili kuyazayunisha maeneo hayo na kuhakikisha unazihodhi na kuzidhibiti kikamilifu ardhi za Wapalestina.

Tags