Hizbullah: Vikwazo vya Marekani havina tofauti na vita vya kijeshi
-
Sayyid Hashim Safiyuddin
Mkuu wa Baraza Kuu la Utendaji la Hizbullah ya Lebanon amesema, vikwazo vya Marekani dhidi ya Lebanon na nchi zingine havina tofauti na vita vya kijeshi.
Vikwazo vya Marekani dhidi ya Lebanon tangu mwaka 2000 vimeinyima na kuikosesha nchi hiyo fursa ya kufanya biashara na nchi zingine; na katika hali hiyo wataalamu wa masuala ya fedha na uchumi wanatahadharisha kuhusu mipango mipya ya Marekani ya kushadidisha hali ya taharuki inayotawala nchini humo.
Kwa mujibu wa ripoti ya Jumapili ya tovuti ya Al-Nashrah, Sayyid Hashim Safiyuddin, Mkuu wa Baraza la Utendaji la Hizbullah ya Lebanon amesema, vikwazo vya Marekani dhidi ya Lebanon na nchi ambazo hazikubaliani na misimamo yake ni aina mojawapo ya vita ambavyo havina tofauti na vita vya kijeshi, na kusudio lake ni kuua na kuangamiza watu.
Safiyuddin amesisitiza kuwa Muqawama utakabiliana na vikwazo hivyo kupitia mipango na suhula zake, ambazo Marekani yenyewe inazifahamu vyema.
Afisa huyo wa Lebanon amekosoa pendekezo lililotolewa na baadhi ya Walebanon kwa Marekani na kusalimu kwao amri mbele ya Washington na akasema, "mapendekezo haya hayatatatua tatizo la Lebanon kuhusiana na kumchagua rais na kuhusiana na masuala ya kiuchumi; na suluhisho pekee la matatizo ya Lebanon ni kuondolewa vikwazo vya Marekani".
Safiyuddin ameongeza kuwa, hatua zote zinazochukuliwa na watu hao zitashindwa na zitagonga mwamba kama zilivyoshhindwa za mabwana zao.
Afisa huyo wa Lebanon amesisitiza pia kuwa, lengo kuu la Hizbullah ni kulinda heshima ya mwanadamu na kuinua sharafu na hadhi yake, tofauti na mhimili wa Magharibi ambao lengo lake ni kumwangamiza mwanadamu katika ngazi zote.
Safiyuddin amebainisha kuwa Hizbullah itatumia suhula zake zote kwa ajili ya kuwahudumia watu wake.
Kabla ya hapo, Sheikh Ali Da'mush, Mkuu wa Baraza la Utendaji la Harakati ya Hizbullah ya Lebanon alisema: "Si muhimu kwa Washington maslahi ya watu wa Lebanon wala kuwepo madarakani rais madhubuti, shujaa na mzalendo; suala muhimu pekee kwa Marekani ni kuona namna gani itaweza kufanikisha maslahi na malengo yake na ya utawala wa Kizayuni wa Israel".
Wabunge wa Lebanon wameshajaribu mara kadhaa kufikia muafaka juu ya uteuzi wa mrithi wa Michel Aoun baada ya kumalizika muhula wa urais wake wa miaka sita, lakini hadi sasa wameshindwa kufanya hivyo, jambo ambalo limezua wasiwasi wa kushadidi mgogoro wa kisiasa nchini humo.../