Vikosi maalumu vya Israel: Hatutahudumu katika jeshi kuanzia Jumapili
Maafisa 100 wa Kikosi cha Akiba cha Oparesheni Maalumu cha utawala wa Kizayuni wa Israel wametangaza kuwa, hawatahudumu jeshini kuanzia Jumapili ijayo wakilalamikia uamuzi wa serikali ya utawala huo wa kubadili muundo wa sheria za mahakama.
Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni wa Israel vimeripoti kuwa wanajeshi wa kikosi cha akiba cha oparesheni maalumu wa Idara za Intelijinsia ya Jeshi, Mossad na Shebah wametoa taarifa ya pamoja wakisisitiza kuwa, Jumapili ijayo sheria ya kwanza ya kidikteta itaidhinishwa, na hiyo itakuwa siku ya kutisha.
Vyombo vya habari vya Kizayuni vimeripoti kuwa, maafisa 100 wa kitengo cha siri cha jeshi la anga la Israel pia wamemwandika barua kamanda wa jeshi hilo kwamba hawatahudumu katika kikosi cha akiba.
Katika wiki za karibuni miito imeendelea kutolewa kati ya wanajeshi wa kikosi cha akiba cha utawala wa kizayuni wakitakiwa kuacha kuhudumu jeshini kutokana na uamuzi uliochukuliwa na Waziri Mkuu wa utawala huo, Benjamin Netanyahu, wa kutekeleza mpango wa marekebisho ya sheria za mahakama ndani ya utawala huo ghasibu.
Mpango huo wa baraza la mawaziri la Netanyahu, unaojulikana kama "marekebisho ya sheria ya mahakama", ambayo wakazi wa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu wanayataja kuwa ni mapinduzi dhidi ya katiba, unapunguza nguvu za mfumo wa mahakama na badala yake unazidisha uwezo na nafasi ya Serikali na Bunge.
Wachambuzi wa mambo wanasema marekebisho hayo yanafanyika kwa shabaha ya kumlinda Benjamin Netanyahu anayeandamwa na kesi kadhaa za uhalifu na ufisadi katika mahakama za Israel.