Walowezi wa Kizayuni wavamia msikiti Nablus, wachoma moto Qurani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i99122-walowezi_wa_kizayuni_wavamia_msikiti_nablus_wachoma_moto_qurani
Walowezi wa Kizayuni wenye misimamo mikali ya kufurutu ada wamevamia msikiti mmoja na kuvunjia heshima Qurani Tukufu katika mji wa Nablus, eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 23, 2023 06:24 UTC
  • Walowezi wa Kizayuni wavamia msikiti Nablus, wachoma moto Qurani

Walowezi wa Kizayuni wenye misimamo mikali ya kufurutu ada wamevamia msikiti mmoja na kuvunjia heshima Qurani Tukufu katika mji wa Nablus, eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Kanda ya kamera ya CCTV imeonyesha namna walowezi hao wa Kizayuni wenye misimamo mikali walivyoshambulia eneo hilo takatifu la Waislamu katika kijiji cha Urif, yapata kilomita 13 kusini mwa Nablus.

Video hiyo imewaonyesha Wazayuni hao waliokuwa wamefunika nyuso zao wakichana na kuchoma moto nakala za Qurani Tukufu ndani ya msikiti huo. Walowezi hao wa Kizayuni hawakuishia hapo, walienda mbali zaidi na kuingiza mbwa ndani ya msikiti huo.

Wakati huohuo, Waziri wa Wakfu na Masuala ya Kidini wa Palestina, Hatem al-Bakri ameonya juu ya kuongezeka vitendo vya walowezi wa Kizayuni wakishirikiana na wanajeshi wa utawala huo pandikizi kuvamia misikiti na kuhujumu matukufu ya Kiislamu katika eneo la Ukingo wa Magharibi.

Amesema kuvamiwa msikiti wa al-Ribat katika kitongoji cha Urif lilikuwa tukio la pili ndani ya siku chache zilizopita. Ametoa mwito kwa Wapalestina wote kuihami misikiti na tasisi za kidini, huku akitoa mwito kwa mashirika ya kimataifa kutekeleza wajibu wao wa kuwawabebesha dhima Wazayuni kwa jinai zao hizo.  

Kabla ya hapo, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ililaani vikali hatua za kigaidi za walowezi wa Kizayuni na wanajeshi wa utawala huo katika baadhi ya maeneo ya Palestina zilizopelekea kuuliwa shahidi raia wa Palestina na kujeruhiwa wengine kadhaa.

Ikumbukwe kuwa, walowezi wa Kizayuni wenye misimamo mikali na wenye silaha juzi Jumatano walivamia kitongoji cha Turmus Ayya huko kaskazini mashariki mwa mji wa Ramallah katika Ukingo wa Magharibi na kisha kuchoma moto magari na nyumba za raia wa Palestina.