Sep 02, 2023 07:33 UTC
  • Vyama 28 vya siasa India kuungana dhidi ya Modi katika uchaguzi wa Mei 2024

Vyama 28 vya upinzani nchini India vimeamua kushiriki kwa pamoja katika uchaguzi mkuu wa 2024 dhidi ya Waziri Mkuu Narendra Modi lengo likiwa ni kuzuia ushindi wa tatu mfululizo wa chama tawala cha Hindu Bharatiya Janata (BJP).

Kambi hiyo ya vyama 28, inayoitwa Muungano wa Kitaifa wa Maendeleo ya Kitaifa wa India, The Indian National Developmental Inclusive Alliance (INDIA), ilitangaza jana kwamba itafanya mipango ya kugawana viti katika majimbo tofauti ili kuzuia kugawanya kura kwa maslahi ya chama cha Modi.

Taarifa iliyotolewa na muungano huo wa kisiasa imesema:"sisi, vyama vya INDIA, tunaazimia kushiriki katika uchaguzi ujao wa Lok Sabha pamoja kadiri tuwezavyo".

Taarifa hiyo imeendelea kueleza kwamba, mipango ya kugawana viti katika majimbo tofauti itaanzishwa haraka na kufikia hitimisho lake mapema zaidi kwa moyo wa ushirikiano wa toa-upewe.

Mkutano wa vyama 28 vilivyoanzisha muungano dhidi ya Narendra Modi 

Viongozi wa chama cha Indian National Congress Sonia Gandhi na Rahul Gandhi jana walijiunga na viongozi wengine wakuu wa upinzani - ikiwa ni pamoja na Sharad Pawar, Arvind Kejriwal, Sitaram Yechury na Lalu Prasad Yadav - katika mkutano wa siku mbili uliofanyika huko Mumbai, mji mkuu wa kifedha na burudani wa India.

Lengo la mkutano huo limetajwa kuwa ni kuanzisha mapambano ya moja kwa moja kwa kuweka mgombea mmoja dhidi ya mgombea wa BJP katika kila wilaya ya uchaguzi.

Uchaguzi mkuu wa taifa wa India umepangwa kufanyika mnamo mwezi Mei mwakani.../

 

Tags