Guterres apongeza azma ya Iran kutuma vikosi vyake kulinda amani duniani
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekaribisha kwa mikono miwili pendekezo la Rais Ebrahim Raisi wa Iran la kuwa tayari wanajeshi wa Jamhuri ya Kiislamu kujiunga na vikosi vya kulinda amani kote duniani.
Mohammad Jamshidi, Naibu Msimamizi wa Ofisi ya Rais wa Iran katika masuala ya kisiasa amesema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa X (Twitter) na kuongeza kuwa, "Dakta Raisi aliwasilisha mapendekezo mawili kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, na mapendekezo hayo yamekaribishwa naye (Katibu Mkuu wa UN)."
Sayyid Raisi aliwasilisha mapendekezo hayo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alipokuwa mjini New York siku chache zilizopita, alikoenda kushiriki Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA.
Jamshidi amesema pendekezo la kwanza la Iran ni kuhusu utayarifu wa vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu kushiriki katika operesheni za kudumisha amani katika pembe mbalimbali za dunia.
Alipokutana na Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa mjini New York Jumatatu iliyopita, Rais wa Iran aliashiria utayarifu wa Jamhuri ya Kiislamu wa kushirikiana na umoja huo katika juhudi zake za kuimarisha usalama na amani duniani, sanjari na kuzuia dhulma dhidi ya mataifa tofauti.
Hii si mara ya kwanza kwa Iran kutangaza azma yake ya kuchangia wanajeshi wake kwenye vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa. Mwaka 2016, Gholam-Ali Khoshrou, aliyekuwa Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa aliliambia Baraza Kuu la UN kwamba, Iran ipo tayari kutoa msaada wa kilojistiki na vikosi vya ulinzi kwa operesheni za jumbe za kulinda amani duniani.
Kwa mujibu wa Jamhidi, pendekezo la pili la Iran ambalo pia limekaribishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ni kuteuliwa wanadiplomasia na wataalamu wa Iran kwenye nyadhifa tofauti kwenye taasisi hiyo ya kimataifa.