Dec 07, 2023 07:06 UTC
  • Guterres atumia Ibara nadra ya UN kutuma ujumbe mzito kwa Baraza la Usalama kuhusu Gaza

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametumia ibara ya 99 ya Hati ya Umoja wa Mataifa, ambayo ni nadra sana kutumiwa na Katibu Mkuu wa umoja huo, kulitolea wito mzito Baraza la Usalama wa "kushinikiza kuepusha janga la kibinadamu" katika Ukanda wa Gaza na kuungana katika kutoa wito wa kusitishwa kikamilifu mapigano kati ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS.

Ibara hiyo ya 99 iliyoko katika Sura ya 15 ya Hati ya Umoja wa Mataifa inasema, mkuu huyo wa UN "anaweza kulijulisha Baraza la Usalama jambo lolote ambalo kwa maoni yake, linaweza kutishia kudumisha amani na usalama wa kimataifa." 

Katika taarifa kwa waandishi wa habari, Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amesema, hii ni mara ya kwanza kwa Guterres kuhisi kwamba analazimika kutumia Ibara ya 99, tangu ashike wadhifa wa Ukatibu Mkuu wa UN mwaka 2017.

Katibu Mkuu wa UN amepigia kelele sana jinai za Israel Gaza

Katika barua yake kwa Rais wa Baraza la Usalama, Guterres amesema, zaidi ya wiki nane za mapigano kwa ujumla "zimesababisha mateso ya kutisha kwa binadamu, uharibifu wa kimwili na kiwewe..."

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameendelea kueleza kuwa, wakati Israel inaendelea kuwalenga wapiganaji wa Hamas, raia katika eneo lote la Ukanda wa Gaza wanakabiliwa na hatari kubwa, huku zaidi ya watu 15,000 wakiripotiwa kuuawa, zaidi ya asilimia 40 wakiwa ni watoto.

Katika sehemu nyingine ya barua yake, Guterres ametahadharisha kuwa, karibuni hivi utulivu wa umma huko Gaza unaweza kutoweka na kusambaratika kikamilifu mfumo wa kibinadamu.

"Hali inazidi kuzorota na kuwa janga lenye athari zisizoweza kurejeshwa katika hali ya awali kwa Wapalestina kwa ujumla na kwa amani na usalama katika eneo," ametanabahisha Katibu Mkuu huyo wa UN na kusisitiza kwa kusema: "matokeo kama haya lazima yaepukwe kwa gharama yoyote."

Iwapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litachagua kuufanyia kazi ushauri wa Guterres na kupitisha azimio la kusitisha mapigano, linao uwezo wa ziada kuhakikisha kwamba azimio hilo linatekelezwa, ikiwa ni pamoja na uwezo wa kuweka vikwazo au kuidhinisha kutumwa kikosi cha kimataifa.

Daniel Forti, mchambuzi mwandamizi wa masuala ya Umoja wa Mataifa katika taasisi ya Kundi la Kimataifa la Migogoro (International Crisis Group) amesema, kwa kuzingatia ukweli kwamba, wenzo huo wa Ibara ya 99 haujawahi kutumiwa tangu mwaka 1989, hatua hiyo ya Katibu Mkuu wa UN inapaza sauti kidiplomasia na kiishara katika duru za umoja huo.

Hata hivyo Forti amekumbusha kuwa, hatua hiyo haitakuwa na taathira kwa mahesabu ya kisiasa ya wanachama watano wenye nguvu zaidi wa Baraza la Usalama.

Inafahamika kuwa Marekani, ambayo ni moja ya madola hayo matano yenye kura ya veto katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa daima hutumia kura hiyo kuzuia maamuzi yoyote yanayokusudiwa kupitishwa na umoja huo dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.../

Tags