Jan 21, 2024 11:25 UTC
  • Mapigano yazuka kati ya majeshi ya Pakistan na Afghanistan kwenye mpaka wa nchi mbili

Mapigano yamezuka kati ya vikosi vya mpakani vya jeshi la Pakistan na vya utawala wa Taliban ya Afghanistan katika eneo la mpaka wa nchi hizo mbili.

Afghanistan na Pakistan zina mizozo ya mpaka, na kumekuwepo na makabiliano ya kila mara kati ya vikosi vya majeshi ya nchi hizo mbili, hali ambayo husababisha kufungwa vivuko vya mpakani mwa nchi hizo mbili.

Wakati huo huo, Islamabad imekuwa siku zote ikiituhumu Afghanistan kwamba inawapa hifadhi magaidi wa Tehreek-e-Taliban ya Pakistan na inasema, magaidi hao wanafanya mashambulio dhidi ya vikosi vya jeshi la Pakistan kutokea kwenye ardhi ya Afghanistan. Hata hivyo Taliban ya Afghanistan inakanusha tuhuma hiyo.

Eneo la mpakani baina ya Pakistan na Afghanistan

Kuhusiana na suala hilo na kwa mujibu wa shirika la habari la Sauti ya Afghan (Ava), mapigano ya mpakani kati ya Pakistan na Afghanistan yalizuka jana Jumamosi asubuhi katika eneo la Ganjgol kwenye kitongoji cha Sarkanu kilichoko mkoani Kunar, mashariki mwa Afghanistan na Bajaur ya Pakistan.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya Afghanistan, ufyatuaji risasi ulianzishwa na vikosi vya mpakani vya Pakistan na ndipo vikosi vya Taliban vikajibu mapigo.

Mapigano hayo yamezuka wakati upande wa Pakistan ulipokuwa ukifanyia matengenezo uzio wa mpaka.

Hakuna ripoti iliyotolewa kueleza kama mapigano na makabiliano hayo yamesababisha maafa ya vifo na majeruhi au la.

Tangu mwaka mmoja nyuma hadi sasa, vivuko vya mpakani kati ya Afghanistan na Pakistan kikiwemo cha Torkham, vingali vimefungwa kwa upitishaji wa bidhaa za kibiashara na za uvukishaji.../

 

Tags