Jan 24, 2024 09:57 UTC

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limefanyika kuhusu suala la vita vya Gaza ambapo mawaziri wa mambo ya nje wa nchi mbalimbali wamekosoa uungaji mkono wa Marekani kwa jinai zinazofanywa na Israel, wakisisitiza udharura wa kusitishwa mauaji ya kimbari dhidi ya Palestina.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov amesema katika kikao hicho cha Baraza la Usalama kuhusu suala la Palestina na Gaza kwamba: Marekani inatumia sera za kinafiki na kindumakuwili kuhusiana na Ukanda wa Gaza na inazuia misaada ya kibinadamu kuingia katika eneo hilo.

Huku akieleza kuwa uingiliaji kati wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi umesababisha maafa, migogoro na vita, Lavrov amesisitiza kwamba: Mpango wa kuwahamisha Wapalestina wa Gaza unatisha na haufai kutekelezwa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema Wapalestina wana haki ya kuwa na serikali na nchi huru, na akasema kwamba Wapalestina hawapaswi kukubali uhandisi wa Marekani kwa ajili ya sura ya taifa la baadaye la Palestina.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Malaysia, Zambry Abdul Kadir, amesema kuwa chombo hicho muhimu cha Umoja wa Mataifa kimeshindwa kusimamisha vita huko Gaza na kuongeza kuwa: 85% ya wakazi wa Ukanda wa Gaza wamefurushwa katika makazi yao, na Israel pia inashambulia shule na makazi ya raia.

UN: Israel inapaswa kukomesha mauaji ya kimbari Ukanda wa Gaza

Waziri wa Mambo ya Nje wa Malaysia amesema, kinachofanywa na Israel katika Ukanda wa Gaza ni mauaji ya kimbari na kuongeza kuwa: Israel lazima iwajibike kwa ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa, kwa sababu utawala huo unawaadhibu Wapalestina kwa pamoja.

Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia, Retno Marsudi amesema katika kikao hicho cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa, utawala ghasibu wa Israel unaendelea kuwaua Wapalestina katika Ukanda wa Gaza na kusema kuwa, upelekaji wa silaha kwa Israel lazima usitishwe, na utawala huo unapaswa kuwajibishwa kwa vitendo vyake.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia amesema lengo la utawala wa Israel ni kuifuta Palestina katika ramani ya dunia na kusisitiza kuwa: Palestina lazima ipate uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa.