Feb 27, 2024 09:47 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Feb 27

Karibu tutupie jicho baadhi ya matukio makubwa ya spoti yaliyojiri katika muda wa siku saba zilizopita kutoka sehemu mbali duniani.....

Iran yamaliza ya 3 Soka ya Ufukweni Asia

Timu ya taifa ya soka ya ufukweni ya Iran imetunukiwa medali ya shaba katika fainali za Kombe la Dunia la Shirikisho la Kandanda Duniani FIFA, baada ya kuichabanga Belarus mabao 6-1 katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu. Katika mechi hiyo ya Jumapili iliyopigwa katika Uwanja Mkuu wa Dubai huko Imarati, vijana wa Iran walionyesha mchezo uliosukwa na uliokwenda shule, na kuishia kuidhalilisha vibaya Belarus. Mabao wa vijana wa Team Melli kama wanavyofahamika hapa nchini yalifungwa na Ali Mirshekari, Movahed Mohammadpour, Mohammad Moradi, Reza Amiri, Mohammad Masoumi na Mohammadali Mokhtari, huko goli la kufutia machozi la Belarus likifungwa na Mikita Chaikouski.

 

Hii ni mara ya pili kwa Iran kutwaa medali ya shaba katika historia ya mashindano hayo ya kandanda ya ufukweni, kwani iliibuka ya tatu pia katika fainali za mwaka 2017. Brazil imeibuka kidedea kwenye mashindano hayo ya dunia ya soka ya pwani 'Beach Soccer' baada ya kuizaba Italia mabao 6-4 katika mchezo wa fainali uliopigwa siku ya Jumapili.

Duru ijayo ya mashindano ya mpira wa miguu unaosakatwa ufukweni itafanyika nchini Ushelisheli mnamo Mei mwaka ujao 2025.

Sepahan nje ya Ligi ya Mabingwa Asia

Klabu ya soka ya Sepahan ya Iran Alkhamisi usiku iliadhibiwa mabao 3-1 na al-Hilal ya Saudi Arabia katika mchuano wa mkondo wa pili wa Ligi ya Mabingwa ya Asia. Licha ya Iran kutangulia kuona lango la wenyeji kupitia goli la Farshad Ahmadzadeh kunako dakika ya 54 ya mchezo, lakini kilichofuata baada ya hapo na msiba. Katika mchuano huo uliopigwa katika Uwanja wa Kingdom Arena mjini Riyadh, wenyeji al-Hilal waliutumia vizuri msemo wa mcheza kwao hutuzwa, na kufanikiwa kucheka na nyavu mara 3 kupitia magoli ya Salem Aldawsari, Ruben Neves na Aleksandar Mitrović. Wiki iliyopita pia, al-Hilal iliizaba Sepahan mabao 3-1 katika mechi ya mkondo wa kwanza wa raundi ya 16 ya Ligi ya Mabingwa Asia mjini Isfahan, katikati ya Iran. Kwa vichapo hivyo, Sepahan imebanduliwa nje ya mechi hizi za kibara.

CAF: Simba yatinga robo fainali kibabe

Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameipongeza klabu ya Yanga kwa kufanya vizuri katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) baada ya kuifunga CR Belouizdad mabao manne kwa sifuri na kufanikiwa kufuzu hatua ya Robo Fainali, akisema mafanikio hayo yameandika historia kubwa kwa klabu na sekta ya michezo nchini. Rais Samia amenukuliwa akisema, "Mmeleta furaha kwa mamilioni ya mashabiki wenu na Watanzania kwa ujumla.” Klabu ya Yanga wikendi ilitinga hatua ya Robo Fainali, Michuano ya Klabu Bingwa Afrika kwa mara ya kwanza katika historia tangu kuanzishwa kwake mwaka 1935, baada ya kuinyoa kwa chupa, tena bila maji CR Belouizdad ya Algeria, kwa kuizaba mabao 4-0 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. Yanga na Beloiuzdad zilikutana tena miezi 3 baada ya mechi ya Hatua ya Makundi ambapo Waarabu walishinda mabao 3-0, na mara hii, Wananchi waliamua kuliza kisasi.

Wekundu wa Msimbazi

 

Mabao ya Yanga kwenye mchuano huo wa Kundi D yalifungwa na Mudathir Yahya, Stephane Aziz Ki, Kennedy Musonda na Joseph Guede Gnadou. Mbali na Yanga, timu nyingine zilizofuzu hatua ya Robo Fainali 2023/24 ya CAF Champions League kufikia sasa ni; Petro Luanda ya Angola, ASEC Mimosas ya Ivory Coast, TP Mazembe ya DRC, Al Ahly ya Misri, na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Watani wa Yanga, Klabu ya Simba nayo iliambulia suluhu ugenini dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast na kufikisha alama 6 kwenye nafasi ya pili nyuma ya Wakodivaa wenye alama 11. Timu hizo zilibanana koo kwenye mchuano huo wa Kundi B na mechi kuishia kwa sare tasa. Simba inatakiwa kushinda mchezo wake wa mwisho kwenye kundi B dhidi ya Jwaneng Galaxy F.C ambao utachezwa tarehe 2 Machi, ili kujihakikishia kucheza Robo Fainali msimu huu.

Kiptum azikwa, mwanariadha mwingine wa Kenya afariki ghafla Cameroon

Ulimwengu wa riadha nchini Kenya umeondokewa na mwanariadha mwingine, Charles Kipsang Kipkorir, majuma mawili baada ya kifo cha mshikilizi wa rekodi ya marathon duniani Kelvin Kiptum. Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Xinhua, Kipsang alifariki dunia Jumamosi, Februari 24, nchini Cameroon. Alianguka na kufa muda mfupi baada ya kumaliza mashindano hayo ya riadha ya kimataifa. Kulingana na vituo vya habari Cameroon, Kipsang alikuwa anashiriki makala ya 29 ya Mount Cameroon Race of Hope. Alikata roho wakati akiendelea kupokea huduma za dharura hospitalani.

Mwendazake Kelvin Kiptum

 

Wakati wa mashindano, Kipsang alikuwa anaongoza kabla ya kukumbwa na matatizo akikaribia utepe. Alimaliza mbio akiwa nafasi ya 16 kama ilivyothibitishwa na Gavana wa Cameroon Bernard Okalai Bilia. Kifo hiki kimejiri majuma mawili baada ya Kenya kumpoteza mwanariadha mwingine wa hadhi ya juu Kelvin Kiptum. Kiptum alifariki katika ajali akiwa na kocha wake Nyarwanda Gervais Hakizimana. Alizikwa kaunti ya Elgeyo Marakwet Ijumaa, Februari 23, 2024 katika mazishi yaliyowaleta pamoja viongozi wa hadhi ya juu serikalini na duniani, akiwemo Rais William Ruto, naibu wake, Rigathi Gachagua na Mkuu wa Mwaziri, Musalia Mudavadi.

Haya yajiri huku, viongozi mbalimbali wakitoa wito kwa serikali na kampuni za vifaa vya michezo kuwajali wanariadha ili kupiga jeki juhudi zao za kuizolea Kenya sifa na medali katika ulingo wa spoti. Wakiongea Ijumaa wakiwa Chepkorio kaunti ya Elgeyo Marakwet, eneo la Bonde la Ufa, katika mazishi ya mshikilizi huyo wa rekodi ya marathon Kelvin Kiptum, viongozi walisema ni wajibu wa serikali na kampuni kama Nike na Golazo kutengeneza miundomsingi eneo pana la North Rift na kuwapa wanariadha vifaa na mazingira mazuri. Waziri wa Michezo wa kenya, Ababu Namwamba aliahidi kwamba maeneo ya North Rift yanaendelea kuimarishwa kwa sababu huko ni kitovu cha wanariadha. “Bidhaa kubwa ya Kenya kwa dunia ni hawa wanariadha wetu,” alisema Bw Namwamba. Kiptum alifariki pamoja na kocha wake Gervais Hakizimana wa kutoka nchini Rwanda, kufuatia ajali ndani ya gari katika barabara ya Eldoret-Eldama Ravine usiku wa Februari 11 kuamkia Februari 12, 2024.

Ligi ya EPL

Na katika Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza, klabu ya Liverpool imesalia kileleni mwa jedwali la ligi ikiwa na alama 60, alama moja zaidi ya Manchester City ambayo wikendi iliizaba Bournemouth bao 1-0. Bao la City kwenye mchezo huo uliopigwa katikak Uwanja wa Vitality lilifungwa na Phil Foden kunadako dakima ya 24 ya mchezo. Arsenal pia wikendi iliishukia vibaya Newcastle na kuigaragaza mabao 4-1 wakiupigia nyumbanji Emirates.

Ligi ya EPL

 

Mabao ya Gunners kwenye mchezo huo yalifungwa na Sven Botman aliyejifunga la kisigino, Kai Havertz, Bukayo Saka na Jakub Kiwior. La kufutia machozi la wageni lilitiwa kimyani na Joe Willock. Kwa ushindi huo, Wabeba Bunduki wanazidi kuchekea katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 58. Manchester United walilimwa mabao 2-1 na Fulham, wakati ambapo Aston Villa ilikuwa inailaza Nottingham Forest mabao 4-2.  

.......................MWISHO.................

 

 

Tags