Mar 23, 2024 02:29 UTC
  • Wito wa maseneta 19 wa Marekani wa kuundwa taifa huru la Palestina

Maseneta 19 wa chama cha Democratic wametoa wito wa kuundwa taifa huru la Palestina katika barua yao iliyotumwa kwa Rais wa Marekani, Joe Biden.

Maseneta hao Marekani wamemtaka Biden kwenda mbali zaidi ya "uwezeshaji" katika mazungumzo ya Israel na Palestina na kuanzisha "mfumo wa kijasiri" wa kuamua hatua zinazofaa za kuanzishwa taifa la Palestina katika Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza. Tom Richard Carpe, ambaye ni mmoja wa washirika wa kisiasa wa Joe Biden na seneta wa jimbo la Delaware, ndiye mbunifu wa barua hiyo.

Wakiongozwa na mpango wa Bill Clinton katika miaka ya 1990, maseneta hao wamesema kuwa, taifa huru la Palestina litakuwa "bila jeshi" ikiwa litaundwa. Maseneta hao wa Marekani pia wametoa wito wa kuwepo mpango wa kuijumuisha Israel katika eneo la Magharibi mwa Asia, wakiashiria juhudi za kuendeleza mazungumzo ya maridhiano kati ya Saudi Arabia na Israel.

Suala la kuundwa taifa la Palestina lisilo na jeshi limejadiliwa kwa muda mrefu, na hata miaka 10 iliyopita, katikati ya mazungumzo na upatanishi wa Marekani ili kutatua mgogoro kati ya Wapalestina na Israel, ilidaiwa kuwa Mahmoud Abbas, mkuu wa Mamlaka ya Palestina, alikubali kuanzisha taifa la Palestina bila jeshi mkabala wa Wapalestina kupewa masuala kadhaa. Hata hivyo mpango huo ulifeli.

Tangu wakati wa uongozi wa George W. Bush, Marekani ililifanya suala la kuundwa mataifa mawili ya Kiyahudi na Palestina kama sera yake kuhusu kadhia ya Palestina kwa kuwasilisha mpango unaopewa jina la "Road Map" au Ramani ya Njia. Hata hivyo, kila mmoja kati ya marais wa Marekani amekuwa na mbinu tofauti katika uwanja huu kulingana na vyama vyao vya Democratic au Republican. Rais wa zamani mdemokrati wa Marekani, Barack Obama, aliunga mkono mpango wa kuwepo dola mbili, ilhali kiongozi wa baada yake, Donald Trump wa chama cha Republican, ambaye alivuka mipaka yote ya hapo awali katika kuinga mkono Israel, alipuuza mpango huo. Trump alijikita zaidi katika kutoa upendeleo, himaya na uungaji mkono wa pande zote kwa utawala wa Tel Aviv na kuzidisha shinikizo kwa Wapalestina. Badala yake, alipendekeza mpango eti wa "Muamala wa Karne" uliojumuisha maeneo yaliyokatwa vipandevipande ya Palestina.

Jambo muhimu ni kwamba, maafisa wa serikali ya Biden wameunga mkono mara kwa mara kuundwa taifa la Palestina bila jeshi kama aina ya suluhisho la kuwepo nchi mbili. Pia, Rais wa Marekani Joe Biden amezungumzia ulazima wa kutekeleza mpango wa kuundwa mataifa mawili ya Kiyahudi na Palestina kutokana na kuwa chini ya mashinikizo ya ndani na nje yanayomtaka abadili mtazamo wake kuhusu Israel. Biden amekuwa akishirikiana kikamilifu na Israel katika mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Gaza.

Sasa, kwa kutilia maanani wito wa maseneta 19 wa Kidemokrati kwa Biden wakitaka kuanzishwa taifa huru la Palestina, inaonekana kwamba suala hili limeingia katika hatua mpya. Barua ya maseneta hao iliandikwa huku mtetemeko wa baada ya ukosoaji mkali wa Chuck Schumer, kiongozi wa Wademokrati walio wengi katika Baraza la Seneti, kuhusu sera za Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni na usimamizi wake wa vita vya Gaza, ukiwa bado unahisika. Katika mahojiano yake na gazeti la New York Times, Schumer kwa mara nyingine tena amemkosoa Netanyahu na kusema: Njia inayofuatwa na utawala wa Tel Aviv ni ya mwinamo mno, ya mporomoko na ya kuangamia. Chuck Schumer amesisitiza kuwa: "Ninaamini kwamba bila msaada wa Marekani, mustakabali wa Israel utafika mwisho." 

Chuck Schumer

Rais wa Marekani, Joe Biden, amemuunga mkono Chuck Schumer, ambaye alimkosoa vikali Netanyahu na kutaka kuitishwa uchaguzi wa mapema huko Israel. 

Katika upande mwingine, Donald Trump amekasirishwa sana na msimamo huo wa Wademokrati. Trump amedai kwamba, Wademokrati wanaidhuru sana Israel. 

Inatazamiwa kuwa msimamo wa sasa wa Wademokrati kuhusu kuundwa taifa huru la Palestina utakabiliwa na jibu kali la utawala wa Kizayuni wa Israel hususan mrengo wa kulia na wenye msimamo mkali ndani ya utawala huo. 

Tags