Mar 23, 2024 11:41 UTC
  • Kula mweleka njama za Marekani za kuunga mkono mauaji ya kimbari ya Israel kwenye UN

Azimio lililopendekezwa na Marekani la kuunga mkono mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel huko Ghaza limegonga ukuta baada ya kupigiwa kura ya veto na Russia na China ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Ni karibu miezi sita sasa utawala wa Kizayuni unaendelea kufanya mauaji ya umati dhidi ya wanawake, watoto wadogo na raia wa kawaida huko Ghaza Palestina. Wapalestina waliothibitishwa kuuawa shahidi kutokana na jinai hizo za Israel hadi hivi sasa ni zaidi ya 33,000. Eneo zima la Ghaza limeharibiwa vibaya na mashambulizi hayo ya kikatili ya Wazayuni. Hivi sasa mgogoro mkubwa wa ukanda huo ni janga la kibinadamu linalotokana na njaa, kiu na maradhi ambalo linawatesa watu hao tena ndani ya mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.

Wakati wananchi wa Ghaza wanaishi katika hali nguvu kama hiyo, Marekani bila ya soni imejitokeza na kuwasilisha muswada wa kuendelea kuunga mkono jinai za Israel. Muswada huo umewasilishwa na Marekani katika hali ambayo hadi hivi sasa Washington imepigia kura ya veto maazimio yote ya kusimamisha mashambulizi huko Ghaza. Katika muswada wa Marekani uliopigwa buti, mbali na kuunga mkono jinai za Israel ulitaka pia Baraza la Usalama liilaani Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS wakati dunia nzima inaona kuwa ni Israel ndiyo inayofanya jinai na mauaji ya kutisha dhidi ya Wapalestina.

Linda Thomas-Greenfield

 

Linda Thomas-Greenfield, mwakilishi wa kudumu wa Marekani ndani ya Umoja wa Mataifa alisema: Haya ni mashambulizi mabaya zaidi kuwahi kufanywa dhidi ya Mayahudi tangu wakati wa Holocaust lakini hakuna mjumbe wa Baraza la Usalama aliyeko tayari kulaani. Naye Antony John Blinken, waziri wa mambo ya nje wa Marekani aliwahi kusema huko nyuma kwamba: Tab'an sisi tuko pamoja na Israel na tunalinda haki zake.

Kwa kweli muswada huo wa Marekani kwa upande mmoja ulikuwa unaunga mkono kuendelea jinai na mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina na kwa upande wa pili kama walivyosema wawakilishi wa Russia na China ndani ya Umoja wa Mataifa, ulikuwa umejaa mambo yasiyoeleweka.

Kabla ya hapo nchi ya Kiafrika ya Algeria ambayo ni mwanachama asiye wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa iliwasilisha muswada wa kutaka Israel ikomeshe mara moja mashambulizi yake huko Ghaza, lakini Marekani bila ya haya iliupigia kura ya veto muswada huo na kuukwamisha. Hivi sasa Algeria nayo imeukataa muswada uliowasilishwa na Marekani wa kuunga mkono jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel. Amar Bendjama, balozi wa Algeria ndani ya Umoja wa Mataifa amesema, matini iliyomo kwenye muswada uliopendekezwa na Marekani haitoshi na haiwasaidii chochote Wapalestina ambao hivi sasa wanateseka kwa hali zote kutokana na jinai za Israel. 

Marekani imewasilisha muswada Umoja wa Mataifa kuunga mkono jinai hizi za Israel dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Ghaza

 

Amma nukta muhimu ya kuzingatia hapa ni kwamba, mwakilishi wa Marekani ndani ya Umoja wa Mataifa anasema kuwa, veto za China na Russia dhidi ya muswada wa nchi yake, zimetokana na ugomvi na ushindani uliopo baina ya madola makubwa duniani. Baada ya nchi za Russia, China na wanachama wengine wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuupiga teke muswada mbovu wa Washington, mwakilishi wa Marekani amesema, Russia na China zimekusudia kwa makusudi kuifelisha Marekani.

Tags