Mar 24, 2024 12:44 UTC
  • Ugaidi, changamoto ya pamoja ya kieneo na wajibu wa kuwa macho

Katika kipindi cha chini ya wiki moja kumetokea miripuko miwili na shambulio kubwa la kigaidi na la umwagaji damu huko Kandahar Afghanistan na kwenye viunga vya mji mkuu wa Russia, Moscow.

Wimbi la kulaaniwa mashambulizi hayo ya kigaidi ni kubwa kiasi kwamba limeushanga ulimwengu na limeonesha jinsi dunia ilivyoshtushwa na mashambulio hayo makubwa ya kigaidi katika kipindi cha siku chache tu. Nukta ya kutiliwa maanani hapa ni kwamba, genge la kigaidi la Daesh (ISIS) limetangaza kuhusika na mashambulizi hayo. Hayo yameshuhudiwa katika hali ambayo kulikuwa na tetesi kwamba genge hilo limeangamizwa kabisa, lakini hivi sasa limejitokeza na kudai kuhusika na mashambulizi makubwa ya kigaidi yaliyopishana kwa siku chache tu huko Kandahar, Afghanista na kwenye viunga vya Moscow, mji mkuu wa Russia. Sasa swali linalojitokeza hapa ni kwamba kuzuka tena jinai hizo kubwa na halafu genge la kigaidi la Daesh kuhusishwa na mashambulizi hayo, kuna maana gani?

Inavyoonekana ni kuwa, genge la kigaidi la ISIS lina malengo kadhaa katika kutangaza kuhusika na mashambulio hayo. Mosi ni kutaka kujionesha kuwa bado lipo na lina uwezo wa kufanya mashambulizi na mauaji katika maeneo tofauti. Pili ni kuzikumbusha nchi za ukanda huu kuwa magaidi hao wameanzisha wimbi jipya la mashambulizi na linaweza kufanya mashambulio makubwa licha ya kuweko hatua kali za ulinzi. 

Magaidi wa Daesh wametangaza kuhusika na mashambulizi mapya ya kigaidi huko Kandahar Afghanistan

 

Baqeri Esmaili ni mchambulizi wa masuala ya kimataifa ambaye kuhusu usuala hili anasema: Inavyoonekana ni kwamba kuzushwa tena jina la Daesh ambalo ni genge katili la kigaidi kunafanyika kwa mpangilio maalumu kutoka kwa waanzilishi na waungaji mkono wa genge hilo na hii inaonesha kuwa, pande zinazolea magaidi bado zina hamu ya kuendelea na vitendo vyao vya kigaidi na mauaji, tena kwa kiwango cha juu.

John Sopko, mwakilishi maalumu wa Marekani nchini Afghanistan amesema kuwa, misaada ya nchi hiyo kwa kundi la Taliban inaishia kwa genge la kigaidi nchini Afghanistan. Mwakilishi huyo wa Marekani ameliita kundi la Taliban kuwa ni la kigaidi na kusema kuwa baada ya kurejea madarakani kundi hilo, Umoja wa Mataifa uliipa Afghanistan msaada wa dola bilioni 2.9. Amesema, sehemu kubwa ya fedha hizo zimetolewa kwa sura ya pesa taslimu na zimeingia mfukoni mwa genge moja la kigaidi.

Tunapoangali hisia zilizooneshwa na wizara ya mambo ya nje na wawakilishi wa Congress ya Marekani baada ya kutolewa matamshi hayo ya Sopko tutaona kuwa, misaada ya Marekani kwa kundi la Taliban ambayo inatolewa kwa madai ya masuala ya kibinadamu, haijulikani inatumika kwenye nini na hata Washington haina taarifa zozote kuhusu zinakokwenda fedha hizo. Cha kushangaza zaidi ni kuwa katika kipindi cha miezi michache tu, mamilioni kadhaa ya dola za Kimarekani yaliingizwa na Umoja wa Mataifa kwenye hesabu ya Benki Kuu ya Afghanistan ambayo tab'an inadhibitiwa na kundi la Taliban. Ni jambo lililo wazi kwamba, fedha hizo haziwezi kutumika kwenye kitu chochote ila kwa idhini ya Taliban.

Marekani ndiyo iliyoanzisha na kulitia nguvu genge la kigaidi la Daesh (ISIS)

 

Alaakullihaal, wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema kuwa, inavyoonekana ni kwamba madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani yameamua kuendelea kutumia magenge ya kigaidi likiwemo la Daesh kama chombo cha kuendeshea operesheni za kigaidi, kuhatarisha usalama wa kieneo na kuzishinikiza nchi zisizokubali kuburuzwa na madola hayo ya Magharibi. Kwa kuzingatia jambo hilo tutaona kwamba ni wajibu kwa nchi za ukanda huu kuwa macho na zinapaswa zishirikiane vizuri zaidi katika kukabiliana na vitendo vya kigaidi na kulinda kwa pamoja usalama wa eneo lao.