Apr 14, 2024 08:15 UTC
  • Maelezo kuhusu baadhi ya silaha zilizotumiwa na Iran dhidi ya Israel

Jumamosi mida ya saa tano usiku kwa saa za Iran au nne na nusu usiku kwa saa za Afrika Mashariki, kitengo cha anga cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kilianzisha rasmi operesheni ya kulipiza kisasi dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel, na kuanzisha mawimbi manne ya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani.

Wimbi la kwanza lilijumuisha makumi ya ndege zisizo na rubani aina ya Shahed-136 za kamikaze au zinazojiangamiza, zilizokadiriwa kuwa takriban 100. Wanaharakati wa mitandao ya kijamii walipiga picha ndege hizo zikiwa katika anga za Iran na Iraq.

Shahed-136 ni ndege isiyo na rubani inaoweza kuruka umbali wa kilomita 2,000 na hubeba bomu lenye uzito wa kilo 50.

Baada ya wimbi la kwanza, mashambulizi mengine matatu ya ndege hizo zisizo na rubani yalifuata kwa muda wa nusu saa, na inakadiriwa kuwa jumla ya ndege zisizo na rubani 400 hadi 500 zilitumika.

Hatua iliyofuata katika operesheni hiyo ya kijeshi ya kulipiza kisasi ilikuwa ni kuvurumishwa makombora ya cruise na balestiki, ambayo yaliripotiwa kuandamana na mashambulio ya wakati mmoja ya ndege zisizo na rubani na makombora ya makundi ya Mhimili wa Muqawama kutoka Iraq, Yemen na Lebanon.

Bado haijatangazwa rasmi ni aina gani za makombora ambayo Iran ilitumia katika operesheni hiyo yenye mafanikio makubwa, ingawa baadhi ya makombora hayo yaliripotiwa kuwa ya Kheibar Shekan.

Kheibar Shekan ni kombora la balestiki la masafa ya kati na lina uwezo wa kuruka umbali wa kilomita 1,450 na kusheheni bomu lenye uzito wa kilo 500.

Kombora la Kheibar Shekan

Iran haijatangaza rasmi maeneo yaliyolengwa, nao utawala wa Kizayuni wa Israel umeamuru watu kutosambaza video za mashambulizi ya Iran.  

Kama ilivyoelezwa kwa usahihi katika uchambuzi wa tovuti ya Press TV, shabaha kuu zilikuwa vituo vya kijeshi vya utawala wa Kizayuni, kuanzia Miinuko ya Golan hadi Jangwa la Negev.

Scott Ritter, mtaalamu wa kijeshi wa Marekani, alisema kwenye jukwaa la X (zamani likijulikana kama Twitter) kwamba angalau makombora saba ya hypersonic ya Iran yalilenga kituo cha jeshi la anga la Israel la Nevatim Air Base na hakuna hata kombora moja lililotunguliwa.

Kambi hii ya jeshi la anga iko katika jangwa la Negev na inahifadhi ndege za Kimarekani za F-35 ambazo zilitumiwa na jeshi katili la Israel katika shambulio la kigaidi kwenye ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus.