Apr 15, 2024 13:42 UTC
  • Vasily Nebenzia
    Vasily Nebenzia

Mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa amekitaja kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na jibu la makombora na ndege zisizo na rubani la Iran dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa ni msimamo wa kinafiki na hadaa wa nchi za Magharibi.

Vasily Nebenzia, ​​amekosoa vikali mienendo ya kinafiki na ya udanganyifu ya Wamagharibi kuhusiana na masuala ya eneo la Magharibi mwa Asia wakati wa kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichojadili jibu la adhabu la Iran kwa utawala wa Kizayuni.

Mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichojadili shambulio la Iran la kulipiza kisasi dhidi ya Israel ni "onyesho la unafiki na mwenendo wa kindumakuwili na wa kuaibisha".

Akiashiria hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kushambulia ubalozi mdogo na kituo cha kidiplomasia cha Iran huko Damascus na hatua isiyofaa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu uhalifu huo, Nebenzia amesema kuwa jibu la Iran halikufanyika bila sababu, bali limetokana na kutochukua hatua kwa Baraza la Usalama kuhusu uhalifu wa Israel huko Damascus.

Baraza la Usalama la UN

Mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa amelitaja chimbuko la mivutano katika eneo la Magharibi mwa Asia kuwa ni uvamizi wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza na kutotekelezwa azimio la Baraza la Usalama la usitishaji vita katika eneo hili.

Wakati huo huo, Nebenzia ameutaka utawala wa Kizayuni kufuata mwenendo wa Iran ambayo haitaki kuzidisha hali ya mivutano na kuepuka matumizi ya nguvu kichochezi katika eneo la Magharibi mwa Asia.

Jumatatu, Aprili 1, 2024, utawala wa Kizayuni wa Israel ulishambulia sehemu ya ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus na kuwaua kigaidi washauri saba wa kijeshi wa Iran.

Jumapili, Aprili 14, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu liliuadhibu utawala huo vamizi kwa kurusha makumi ya ndege zisizo na rubani na makombora kuelekea maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Palestina (Israel).