Umoja wa Mataifa: Watoto wanakabiliwa na wimbi la ukatili
(last modified Thu, 10 Oct 2024 11:27:58 GMT )
Oct 10, 2024 11:27 UTC
  • Umoja wa Mataifa: Watoto wanakabiliwa na wimbi la ukatili

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, tabaka la watoto linakabiliwa na wimbi la ukatili katika maeneo mbalimbali ulimwenguni.

Hayo yameelezwa na mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili dhidi ya watoto na kutahadharisha juu ya ongezeko kubwa la vitendo hivyo.

Najat Maalla M'jid, mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili dhidi ya watoto ameonya kwamba, vijana wanakabiliwa na wimbi la ukatili na unyanyasaji wa kijinsia ambao haujawahi kushuhudiwa.

Ukatili huo unasababishwa na vita, mabadiliko ya hali ya hewa, njaa pamoja na uhamishwaji.

Najat Maalla M'jid, mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ukatili dhidi ya Watoto ameongeza kusema kuwa, watoto hawahusiki na vita, wala migogoro lakini wanapitia changamoto kubwa.

Najat Maalla M'jid, mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ukatili dhidi ya Watoto 

 

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa aleo alitarajiwa kuwasilisha ripoti yake katika mkutano wa Umoja wa Mataifa inayoonyesha jinsi ukatili dhidi ya watoto ulivyoenea, na kwamba teknolojia inawezesha uhalifu dhidi ya vijana kuliko hapo awali.

Ripoti hiyo inaonyesha kwamba zaidi ya watoto milioni 450 waliishi katika maeneo yenye migogoro kufikia mwishoni mwa 2022, asilimia 40 ya watu milioni 120 waliokimbia makazi yao mwishoni mwa Aprili walikuwa watoto, na watoto milioni 333 wanaishi katika umaskini uliokithiri.

Vitendo vya ukatili dhidi ya watoto viliripotiwa kuongezeka sana mwaka jana (2023) katika maeneo yanayoshuhudia vita na mapigano.

Hayo yamo katika ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa inayoeleza ukatili dhidi ya watoto katika maeneo yaliokumbwa na migogoro kwa mwaka 2023. Ripoti hiyo inabainisha juu ya kuongezeka sana ukatili dhidi ya watoto kuanzia Palestina kufuatia mashambulio ya Israel dhidi ya Gaza hadi Sudan, Myanmar na Ukraine.