Jul 22, 2016 10:27 UTC

Waislamu wa eneo la Kashmiri lililoko chini ya India wamefanya maandamano makubwa ya kulaani serikali ya India baada ya jeshi la nchi hiyo kuwaua baadhi ya wanaharakati wanaopigania uhuru wa eneo hilo.

Huku hayo yakiripotiwa, mwanachuoni wa Kisunni ambaye pia ni mjumbe wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran linalomchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ametoa wito kwa Waislamu kote duniani kulaani mauaji ya hivi karibuni ya ndugu zao wa eneo la Kashmir linalodhibitiwa na India.

Sheikh Molavi Ahmad Salami amewataka Waislamu kuonyesha uungaji mkono wao kwa ndugu zao wa Kashmiri na kusisitiza kuwa, kadhia ya eneo hilo linalodhibitiwa na India imeendelea kufumbiwa macho na ulimwengu wa Kiislamu kama kadhia ya Palestina.

Mwanachuoni wa Kisunni nchini Iran, Sheikh Molavi Ahmad Salami

 

Mwanachuoni huyo wa Kisunni wa nchini Iran ameongeza kuwa, ni jukumu la kila Muislamu kusimama na kupinga dhulma na mateso wanayopitia Waislamu wa Kashmir. Amesisitiza kuwa, katika hali ambayo haifai kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine, lakini wapenda haki duniani na haswa nchi za Kiislamu zina wajibu wa kuwaunga mkono kisiasa Waislamu wa Kashmir.

Waislamu wa Kashmiri waliotelekezwa na ulimwengu wa Kiislamu, hawana wa kumlilia ila Muumba wao

 

Watu wasiopungua 45 wameuawa katika machafuko yaliyoanza Julai 9 katika eneo hilo huku wengine 3,500 wakijeruhiwa, baada ya jeshi la India kutumia nguvu kupita kiasi kuwakandamiza waandamanaji ambao wamekuwa wakitoa nara za kutaka uhuru.

Kashmir ni jimbo lenye Waislamu wengi India na limekuwa likikumbwa na mzozo tokea India ipate uhuru kutoka Uingereza mwaka 1947.

Tags