Iran na Misri zataka Israel ilazimishwe kukomesha jinai zake Gaza, Lebanon
(last modified Thu, 24 Oct 2024 06:18:44 GMT )
Oct 24, 2024 06:18 UTC
  • Iran na Misri zataka Israel ilazimishwe kukomesha jinai zake Gaza, Lebanon

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian na mwenzake wa Misri, Abdel Fattah El-Sisi wamesisitiza kuwa uchokozi wa Israel katika Ukanda wa Gaza na Lebanon ni lazima usitishwe, na kutoa wito wa kuwepo juhudi za kuzuia kuenea kwa mzozo katika maeneo mengine ya eneo la Asia Magharibi.

Pezeshkian na El-Sisi walikutana jana Jumatano katika mji wa Kazan nchini Russia, ambako wanahudhuria mkutano wa kilele wa kundi la nchi zinazoinukia kiuchumi za BRICS.

Rais wa Iran amesisitiza kuwa, kuimarisha uhusiano na nchi za kanda ni kipaumbele cha serikali yake. "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haifuatilia vita au migogoro kwa njia yoyote ile," ameongeza Dakta Pezeshkian.

Hata hivyo, Rais wa Iran ameonya kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itatoa jibu la "kuumiza" iwapo utawala haramu wa Israel utafanya makosa kwa kuishambulia Iran.

"Kimsingi, utawala huo (wa Kizayuni) unaweza kuisababisha madhara Iran, lakini madhara ambayo utayapokea kutokana na jibu (la Iran) hayatasawiriki," ameeleza bayana Rais wa Iran.

Rais wa Misri kwa upande wake ametoa wito wa umoja miongoni mwa mataifa ya Kiislamu. "Lazima tushirikiane ili kusaidia kumaliza vita Gaza na Lebanon, na kuzuia kuenea kwa migogoro katika maeneo mengine," ameongeza El-Sisi.

Tags