Taarifa ya Europol kuhusu kushadidi harakati za kigaidi barani Ulaya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i12070-taarifa_ya_europol_kuhusu_kushadidi_harakati_za_kigaidi_barani_ulaya
Polisi ya Ulaya (Europol) imetangaza kuwa mamia ya magaidi wamejitayarisha kwa ajili ya kufanya mashambulizi barani Ulaya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 27, 2016 02:08 UTC

Polisi ya Ulaya (Europol) imetangaza kuwa mamia ya magaidi wamejitayarisha kwa ajili ya kufanya mashambulizi barani Ulaya.

Europol imetangaza kuwa magaidi wanaopigana katika nchi za Iraq na Syria kwa ajili ya kundi la Daesh wameanza kurejea Ulaya. Europol imesema kuwa, makundi ya kigaidi na yale yenye misimamo mikali yanaingia Ulaya kwa kutumia hati bandia au za kweli za kusafiria na wala hayategemei magenge ya magendo ya binadamu. Taarifa ya Europol inakadiria kuwa, magaidi kutoka Ulaya wanaopigana katika kundi la kigaidi la Daesh huko Iraq na Syria ni elfu 5 na karibu 1500 hadi 1800 wamerejea Ulaya.   

Taarifa mpya ya Europol kuhusu ongezeko la vitisho vya kigaidi barani Ulaya inapata maana kwa kutilia maanani silisila na mfululizo wa mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea hivi karibuni katika nchi kubwa za bara hilo hususan Ufaransa na Ujerumani. Shambulizi kubwa la kigaidi la hivi karibuni zaidi ni lile la tarehe 14 mwezi huu wa Julai ambapo mtu anayedhaniwa kuwa mwanachama wa kundi la kigaidi la Daesh alishambulia umati wa watu katika mji wa Nice kwa kuwagonga kwa lori na kuua 84 miongoni mwao. Watu wengine zaidi ya 200 walijeruhiwa. 

Kwa sasa ni jambo linalotazamiwa kutokea mashambulizi ya kigaidi barani Ulaya wakati wowote ule. Ukweli huo unatiwa nguvu na matamshi ya Waziri Mkuu wa Ufaransa, Manuel Valls ambaye amewataka raia wa nchi hiyo wajitayarishe kwa mashambulizi zaidi kama hayo.

Magaidi wa Daesh na waitifaki wao

Jambo la kutiliwa maanani ni kuwa, viongozi na taasisi za usalama za Ulaya zinazungumzia suala la kuongezeka vitisho vya ugaidi barani humo wakati zinajua vyema kwamba, baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya hususan Ufaransa na Uingereza pamoja na Marekani na waitifaki wake wa Kiarabu, zilikuwa na mchango mkubwa na muhimu katika kuanzisha na kuliimarisha kundi la kigaidi la kiwahabi la Daesh na makundi mengine ya kigaidi huko Syria. Matokeo ya mwenendo huo yanaonekana waziwazi barani Ulaya katika sura mbili. Kwanza ni wimbi kubwa la wakimbizi wanaomiminika barani Ulaya ambalo limeutumbukiza Umoja wa Ulaya katika mgogoro mkubwa zaidi tangu kuanzishwa kwake. Matokeo ya pili ya mwelekeo huo ni kupanuka kwa harakati za kigaidi barani Ulaya baada ya magaidi walioruhusiwa hapo awali kwenda Syria kwa shabaha ya kuiondoa madarakani serikali halali ya nchi hiyo kuanza kurejea makwao. Watu wa Ulaya hawakudhani hata kidogo kwamba misaada yao katika kuanzisha na kuliimarisha kundi la Daesh na makundi mengine ya kigaidi itakuwa na mwangwi mbaya utakaorejea huko huko Ulaya na kuwa tishio kubwa kwa watu wa eneo hilo.  

Shambulizi la kigaidi Nice, Ufaransa

Ukweli ni kwamba, nchi za Ulaya sasa zinavuna matunda ya mche zilioupanda zenyewe. Mashambulizi ya hivi karibuni katika miji ya Nice na Paris nchini Ufaransa na vilevile mashambulizi ya kigaidi ya Machi mwaka huu mjini Brussels huko Ubelgiji ni matokeo ya kutumia ugaidi kama wenzo wa kufikia malengo na vilevile hatua ya baadhi ya nchi za Magharibi ya kuugawa ugaidi katika ugaidi mzuri na mbaya.

Wapiganaji wa kiwahabi wa Daesh

Nchi za Magharibi na waitifaki wao wa Kiarabu badala ya kukabiliana na aina zote za ugaidi wa makundi ya kitakfiri na kiwahabi zimeyatumia makundi hayo kwa shabaha ya kutimiza matakwa na malengo yao katika nchi kama Syria na Iraq na matokeo yake magaidi hao sasa wamewageukia mabwana zao na kuanza kuwang'ata.